*Tanga kuwa Kitovu cha Nishati Afrika Mashariki
Serikali ya Tanzania na Uganda zinatarajia kujenga Kituo Kikubwa cha Kusafisha Mafuta Ghafi katika Mkoa wa Tanga nchini Tanzania na kuifanya Tanga kuwa kitovu cha Nishati (Energy Hub).
Hayo yameelezwa na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kabuta Museveni wakati wa uzinduzi wa matanki ya kuhifadhi mafuta nchini Uganda uliofanyika tarehe 17 Septemba 2026 , katika mji wa Kampala nchini Uganda ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta wa Tanzania, Dkt James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) Mussa Makame na Kamishina wa Mafuta Wizara ya Nishati Godluck Shirima walialikwa.
Museveni amesema mradi huo ni ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ambapo hatua hiyo ni kuimarisha usalama wa mafuta katika Ukanda wa Afrika Mashariki, hususani Tanzania na Uganda ambapo mafuta hayo yatatoka nchini Uganda na mengine kutoka nchi zinazozalisha mafuta ya aina hiyo.
Museveni amebainisha kuwa mbali na kituo hicho kikubwa kujengwa Tanzania pia kutajengwa kituo kidogo cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta wa Tanzania, Dkt James Mataragio, amesema kuwa kujengwa kwa kitovu cha Nishati mkoani Tanga ni fursa kwa Tanzania kujitangaza , kuhamasisha na kuchochea maendeleo katika nchi za Kusini mwa Afrika( SADIC).
Vilevile amesema uwekezaji wa miradi hiyo mikubwa ya mafuta nchini Tanzania, ni kuhamasisha usalama wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta katika nchi za kusini mwa Afrika (SADIC).
Ikumbukwe kuwa nchi hizo mbili kwa sasa zinatekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka eneo la Hoima nchini Uganda hadi Tanga katika eneo la Chongoleani(ECOAP) ambapo utekelezaji wake umefikia 92% na Desemba mwaka huu utakamilika na mafuta kuanza kusafirishwa katika mabomba husika.






