Na OWM–TAMISEMI, Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewaagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Waziri wa Maliasili na Utalii kufika ndani ya siku saba katika Dampo la Pugu kwa ajili ya kutatua mgogoro wa muda mrefu wa wananchi kuhusu mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo Septemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wananchi wa Pugu mara baada ya kufanya ziara katika Dampo la Pugu, linalohudumia Mkoa wa Dar es Salaam kwa kupokea taka, na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi wa eneo hilo.
“Nikiwa Dampo kuna wazee wangu waliwasilisha malalamiko juu ya kubuguziwa katika Msitu wa Kazimzumbwi, wakidai hawajui kama wako eneo gani la utawala, Pwani au Dar es Salaam. Hivyo, ninawaelekeza Mawaziri wa TAMISEMI, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wa Maliasili na Utalii kuhakikisha ndani ya siku saba wawe wamefika hapa kutatua changamoto hiyo ya wananchi kubuguziwa,” amesema Mhe. Ndejembi.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka mawaziri hao watakapofika katika eneo hilo kuzungumza na wananchi na kuhakikisha katika kutatua changamoto hiyo wanatumia taarifa rasmi ya Serikali kuhusu mipaka ya kiutawala, yaani Government Notice (GN) iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali, kama msingi wa kubaini mipaka husika.
Akizungumza kwa niaba ya mawaziri wenzake, Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameahidi kutekeleza maelekezo hayo ya Makamu wa Rais kwa kufika katika eneo hilo ndani ya siku saba na kuzungumza na wananchi kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo.
“Mhe. Makamu wa Rais, tumepokea maelekezo yako ya kutatua mgogoro huu wa wananchi wa mipaka ya kiutawala na Msitu wa Kazimzumbwi ndani ya siku saba. Hivyo, mimi Prof. Riziki Shemdoe, Waziri wa TAMISEMI, Dkt. Akwilapo, Waziri wa Ardhi, na Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Maliasili, tutakuja kuzungumza na wananchi ili kutatua mgogoro huo,” amesema Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe ameahidi kutekeleza maelekezo ya Makamu wa Rais ya kuzisimamia Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam kuleta vitendea kazi, ikiwemo tingatinga (bulldozer), kwa ajili ya kuboresha mazingira na kuongeza ufanisi wa huduma ya upokeaji wa taka katika Dampo la Pugu.
Prof. Shemdoe amesema tayari amemwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanza kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo ili kuhakikisha vitendea kazi vinapatikana na hatua zinazohitajika zinachukuliwa.
Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa kufanya ziara katika Dampo la Pugu, kusikiliza kero za wananchi na kutoa maelekezo ya hatua za haraka kuchukuliwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa dampo hilo linalohudumia Mkoa wa Dar es Salaam.












