*Balozi Deo Mwapinga afanikisha mkutano mkubwa Dar

*Dk. Tulia ashauri wanawake viongozi uwepo wao utambuliwe

*Dk. Mihayo wa TCB asema wanawake ni waaminifu, wakikopa wanarejesha

Na Deodatu Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tanzania inatarajia kuwa kitovu cha diplomasia ya kibunge barani Afrika mwezi Novemba, mwaka huu, itakapowakaribisha wabunge wanawake na viongozi mashuhuri kutoka nchi 12 wanachama wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR).

Mkutano huu mkubwa, utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa wa Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika nyanja za amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi kwa mwanamke wa ukanda huu.

Katika hafla ya uzinduzi wa maandalizi ya mkutano huo iliyofanyika hivi katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam, Septemba 18, 2026, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Barron Sillo, alitangaza rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, atakuwa Mgeni Rasmi katika mkutano huo utakaofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 5 Novemba 2026.

Sillo alibainisha kuwa uamuzi wa Tanzania kuwa mwenyeji unaakisi historia ya nchi hii kama kisima cha amani tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo mwaka 2004 kupitia Azimio la Dar es Salaam.

“Tanzania tunatambua kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa na vyombo vya kufanya maamuzi ni msingi wa demokrasia jumuishi. Kwa sasa, bunge letu lina asilimia 40 ya wabunge wanawake, takwimu inayotufanya kuwa nchi ya nne kati ya nchi 12 za ukanda huu,” alisema Sillo

Ameongeza kuwa mkutano huo utakuwa fursa ya kipekee ya kuimarisha diplomasia ya kibunge na kutafuta suluhu za kudumu kwa changamoto zinazoukabili ukanda wa maziwa makuu.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amekumbusha kuwa safari ya Tanzania katika kumuwezesha mwanamke ina mizizi mirefu, kuanzia harakati za Bibi Titi Mohammed hadi kufikia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk. Gwajima amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1325 kupitia Mpango Kazi wa Kitaifa (2023-2027).

“Haitoshi tu kuwa na historia pekee, bali tunapaswa kuhakikisha historia hiyo inageuka kuwa sera, sheria na bajeti zinazoleta matokeo kwa wanawake na wasichana. Tunataka maazimio yatakayofikiwa mwezi Novemba yajulikane na yatekelezwe kwa vitendo,” amesisitiza Dk. Gwajima.

Umuhimu wa mkutano huu pia uliungwa mkono na Dk. Tulia Ackson, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Tanzania mstaafu.

Dk. Tulia amefanya uchambuzi wa kina kuhusu haja ya wanawake kuhama kutoka kwenye “kuwepo” tu (presence) hadi kuwa na “ushawishi wa kweli” (influence).

Amebainisha kuwa amani inadumu pale tu ambapo haki za binadamu zinaheshimiwa, na wanawake wana nafasi ya pekee ya kuzungumzia masuala ya watoto, elimu na afya kama misingi ya amani.

“Ili wanawake wawe na ushawishi wanapoketi mezani, lazima wajipambanue. IPU itashirikiana kwa karibu na mkutano huu wa Novemba ili kuhakikisha ahadi zinazotolewa zinatafsiriwa kuwa programu zinazoweza kutekelezeka na kuleta matokeo yanayogusika.”

Ameonyesha jinsi IPU inavyoweza kusaidia kanda hii kutafsiri ahadi za kimataifa kuwa sheria za kitaifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja huu, Balozi Dk. Deogratias Mwapinga ameutaja mkutano huu wa FP-ICGLR kuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya jukwaa hilo.

Chini ya uongozi wake, jukwaa limekuwa daraja imara la ushirikiano kati ya mabunge ya nchi 12, likizingatia masuala nyeti kama suluhu za wakimbizi, uraia na utulivu wa kikanda.

Maandalizi ya mkutano huu ni ushahidi mwingine wa jinsi Balozi Mwapinga alivyofanikiwa kuimarisha jukwaa hilo kama chombo cha kutetea amani na usalama.

Katika mwelekeo wa kiuchumi, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Dk. Adam Mihayo, naye ametoa uchambuzi mzito wa kwanini sekta binafsi ina wajibu wa kimkakati kumuwezesha mwanamke.

Dk. Mihayo ametumia mfano wa Kaskazini mwa Uganda, ambapo baada ya vita, wanawake walichukua jukumu la kufufua uchumi, na sasa wanamiliki asilimia 70 ya biashara ndogo na za kati katika eneo hilo.

Mihayo alieleza kuwa TCB imejipanga kikamilifu kumkomboa mwanamke kwa vitendo.

Ametoa takwimu za kutia moyo: “Katika TCB, asilimia 30 ya mikopo tuliyotoa nchini Tanzania ni kwa biashara zinazoendeshwa na wanawake, yenye thamani ya shilingi bilioni 540.

“Jambo la kustaajabisha ni kwamba, wakati uwiano wa mikopo isiyolipika (NPL) kwa ujumla ni asilimia 3.5, kwa wanawake ni chini ya asilimia 1.5.”

Uchambuzi huu wa Mihayo unaonyesha kuwa mwanamke si tu ni mzalishaji, bali ni mkopaji mwaminifu anayehakikisha fedha zinadumu na kuleta tija.

Amehusisha juhudi hizi na Dira ya Taifa ya 2050, inayolenga kutokomeza umaskini uliokithiri kupitia makundi maalum ya wanawake na wenye ulemavu.

“Kumuwezesha mwanamke si jambo la kiungwana tu; ni uwekezaji wenye faida kubwa kiuchumi ambao unaimarisha ajira na kupanua wigo wa kodi kwa taifa letu,” ameongeza Mihayo.

Mkutano huu wa Novemba si tu utakuwa jukwaa la mazungumzo, bali ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu katika kuleta amani ya kudumu kupitia nguvu ya mwanamke.

Kwa uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan kama mgeni rasmi, na ushiriki wa viongozi kama Mhe. Judith Suminwa, Waziri Mkuu wa DRC, mkutano huu unatarajiwa kuacha alama ya kudumu katika historia ya ukombozi wa mwanamke barani Afrika.

Kama alivyohitimisha Dk. Mihayo, changamoto kubwa iliyopo mbele ya viongozi wa ukanda huu ni “utekelezaji”.

Mkutano huu unatarajiwa kutoa majibu ya vitendo jinsi ya kuimarisha ulinzi wa wanawake, kukuza amani na kuhakikisha mwanamke anakuwa injini ya maendeleo ya kiuchumi kuelekea mwaka 2050.

Tanzania ipo tayari, na ukanda wa Maziwa Makuu upo tayari kuanza ukurasa mpya wa ushirikiano na ustawi.