*Rukwa wajipanga kufanikisha kwa kishindo

*Dk Mapana asifu utayari Rukwa

Na Innocent Byarugaba -ORMV, Rukwa

Mkoa wa Rukwa umefikia asilimia 80 ya maandalizi ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitakachokwenda sambamba na Kumbukizi ya Miaka 27 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana Kitaifa, kinachotarajiwa kufanyika Oktoba 14, 2026 kwenye kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga.

Hatua hiyo imebainika wakati kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi kilichoongozwa na Katibu wa Mkoa wa Rukwa Msalika Robert Makungu kikiwaunganisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais maendeleo ya Vijana,Wizara ya Ajira na Uwezeshaji Vijana Zanzibar walipotembelea na kukagua maeneo muhimu yatakayotumika katika shughuli hizo, ikiwemo Uwanja wa Nelson Mandela, Uwanja wa Ndua,eneo litakakofanyika kongamano la Wiki ya Vijana Kitaifa na maandalizi ya halaiki.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Wizara ya Maendeleo ya Vijana, Dkt. Kedmon Elisha Mapana, amepongeza hatua iliyofikiwa na kusisitiza kuendelea na kasi hiyo ili kukamilisha maandalizi wakati na viwango vinavyohitajika

Aidha, maandalizi ya halaiki yanaendelea kwa kushirikisha vijana 1500 na makundi mbalimbali, yakilenga kuonesha vipaji, ubunifu na ujumbe wa kizalendo kupitia sanaa na maonesho.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Ajira na Uwekezaji Zanzibar, Khalid Maulid Waziri, amepongeza ushirikiano wa viongozi, watendaji, vijana na wananchi wa Rukwa, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kufanikisha tukio hilo la kitaifa lenye sura ya muungano

Akizungumza na Vyombo vya habari Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Makongoro Nyerere amesema tukio hilo kwa Mkoa wa Rukwa ni heshima kubwa, fursa ya Kiuchumi hivyo Wananchi wameonesha furaha na utayari wa kuwapokea wageni ambao watachochea shughuli za kiuchumi na kuwapa vijana fursa mbali mbali za ajira.

Mwenge wa Uhuru utapokelewa rasmi Mkoani Rukwa tarehe 10 Oktoba,2026 na kukimbizwa kwenye Halmashauri zake 4 ambapo tarehe 14 Oktoba, 2026 utafikia kilele huku Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.