Na Stella Aron, JamhuriMedia

Serikali imeanza kuimarisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa kuweka mkazo katika utabiri unaolenga hatua, unaolenga kuwasaidia wananchi na wadau kutafsiri taarifa za hali ya hewa na kuchukua hatua mapema kabla ya kutokea kwa majanga.

Hatua hiyo inalenga zaidi kulinda sekta za kilimo na mifugo ambazo ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na athari kubwa za matukio ya hali ya hewa kama ukame, mafuriko, joto kali, upepo mkali pamoja na wadudu na magonjwa yanayoathiriwa na hali ya hewa.

Msisitizo huo umetolewa mjini Morogoro wakati wa uzinduzi wa programu ya WISER ActionFirst™, iliyoambatana na warsha ya kitaifa ya siku tatu ya ushirikishwaji wa wadau katika kuandaa taarifa mahususi za hali ya hewa kwa sekta za kilimo na mifugo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, anasema kuna umuhimu wa kuondoka katika mfumo wa kutoa taarifa zinazoeleza tu hali ya hewa inayotarajiwa na kuelekea katika mfumo unaoeleza pia athari zinazoweza kujitokeza na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Kwa mujibu wa Ndagala, taarifa za utabiri zinapaswa kumsaidia mtumiaji kufahamu si tu hali ya hewa itakavyokuwa, bali pia nini kifanyike, nani achukue hatua, wapi na kwa wakati gani.

Anasema Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Menejimenti ya Maafa, inaendelea kuratibu juhudi za kitaifa za kuzuia na kupunguza madhara ya maafa, kujiandaa, kukabiliana nayo na kurejesha hali baada ya maafa kutokea.

Katika utekelezaji wa jukumu hilo, alisema ushirikiano na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni muhimu ili kuhakikisha taarifa za utabiri na tahadhari zinatumika katika kufanya maamuzi na kuchukua hatua kabla ya madhara kutokea.

GHARAMA ZA MAJANGA

Umuhimu wa hatua hiyo unaonekana katika athari zinazotokana na majanga yanayohusiana na hali ya hewa, hasa katika kilimo na mifugo.

Ndagala anasema sekta hizo ni tegemeo la maisha na shughuli za kujipatia kipato kwa zaidi ya robo tatu ya Watanzania, huku zikiwa katika hatari ya kuathiriwa na ukame, mafuriko, vipindi virefu vya ukavu, joto kali na upepo mkali.

Anasema matukio hayo yanaweza kupunguza uzalishaji na usalama wa chakula, huku yakiongeza mzigo katika bajeti ya Serikali kutokana na gharama za kukabiliana na majanga na kurejesha hali.

Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, wastani wa hasara za kila mwaka zinazohusishwa na mafuriko unatarajiwa kuongezeka kutoka dola za Marekani milioni 28 hadi milioni 41, wakati hasara zinazohusishwa na ukame zikitarajiwa kuongezeka kutoka dola milioni 140 hadi milioni 350.

Morogoro ni miongoni mwa maeneo yaliyowahi kukumbwa na athari hizo. Ndagala anasema mafuriko yaliyohusishwa na El Niño mwaka 2019 na 2023/24 yaliathiri takribani hekta 30,000 hadi 36,000 za mpunga na mahindi katika Bonde la Mto Kilombero, huku tathmini ya hasara ya mazao ikiwa takribani dola milioni 69.

Katika upande wa mifugo, anasema ukame wa mwaka 2021/22 uliua zaidi ya mifugo 92,000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Aidha, tathmini ya hasara na uharibifu unaohusishwa na ukame katika maeneo ya Ngorongoro, Longido na Monduli imeonesha thamani ya takribani dola milioni 80.

Hali hiyo imeifanya Serikali kuweka mkazo katika hatua za kinga na tahadhari za mapema, badala ya kusubiri majanga yatokee ndipo rasilimali zitumike kukabiliana na madhara.

Ndagala anasema kati ya Mwaka wa Fedha 2024/25 hadi Aprili 2026, Serikali ilitumia shilingi bilioni 904.221 katika kukabiliana na majanga.

TMA KUBORESHA TAARIFA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a, anasema programu hiyo inalenga kuongeza matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa kuandaa utabiri unaozingatia mahitaji ya watumiaji, hususan katika sekta za kilimo na mifugo.

Chang’a anasema TMA, ambayo pia inatekeleza jukumu la kuwa Kituo cha Kitaifa cha Tahadhari za Mapema, imekuwa ikitoa taarifa kuhusu matukio hatarishi ya hali ya hewa, yakiwemo mvua kubwa, upepo mkali, mawimbi makubwa, joto kali na vimbunga vya kitropiki.

Anasema TMA tayari imepiga hatua katika utoaji wa Utabiri Unaozingatia Athari (Impact-Based Forecasting) kwa sekta mbalimbali, lakini matumizi ya utabiri huo katika kilimo na mifugo bado ni madogo.

Kutokana na hali hiyo, anasema programu ya WISER ActionFirst™ inalenga kuendelea kuboresha taarifa za hali ya hewa ili ziweze kutumiwa moja kwa moja katika kufanya maamuzi na kuchukua hatua za mapema.

Anasema mpango huo pia utaongeza thamani katika huduma zilizopo na kuchangia katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma muhimu za tahadhari za mapema.

WADAU WASHIRIKISHWE

Mkurugenzi wa Ofisi ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Kanda ya Afrika, Dkt. Agnes Kijazi, anasema kutoa utabiri pekee hakutoshi kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa wakati.

Anasema mafanikio ya mfumo wa tahadhari za mapema yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi zinazotoa huduma za hali ya hewa, menejimenti ya maafa, wizara za kisekta, wadau wa kibinadamu, vyombo vya habari na jamii zilizo katika hatari.

Kwa mujibu wa Kijazi, uandaaji shirikishi wa taarifa utasaidia kuziba pengo lililopo kati ya taarifa za utabiri na hatua za mapema kwa kuhakikisha tahadhari zinaandaliwa kwa kuzingatia mahitaji na maoni ya watumiaji.

Anasema mchakato huo utasaidia kuimarisha uratibu kati ya huduma za utabiri na sekta za kilimo na mifugo, kuboresha utabiri unaozingatia athari na kuandaa hatua mahususi zinazoweza kutekelezwa kabla ya madhara kutokea.

Kijazi anasema ushirikishwaji wa wadau kuanzia ngazi ya taifa hadi jamii ni muhimu ili kuhakikisha taarifa zinazoandaliwa zinaendana na mazingira na mahitaji halisi ya maeneo husika.

TAHADHARI KUWAFIKIA WALIO HATARINI

Warsha hiyo imewakutanisha wataalamu wa hali ya hewa, waratibu wa maafa, maafisa ugani, watafiti, vyombo vya habari, mamlaka za serikali za mitaa, wakulima na wafugaji kwa lengo la kubaini majanga ya kipaumbele na kutathmini athari zake katika sekta za kilimo na mifugo.

Washiriki pia wanajadili maamuzi muhimu yanayopaswa kuchukuliwa kabla ya madhara kujitokeza, muda wa kujiandaa na njia bora za mawasiliano zitakazowezesha utekelezaji wa hatua za tahadhari.

Aidha, msisitizo umewekwa katika kuhakikisha taarifa zinawafikia makundi yaliyo katika mazingira hatarishi zaidi, yakiwemo wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na jamii za wafugaji.

Kwa mtazamo huo, utekelezaji wa programu ya WISER ActionFirst™ unalenga kuimarisha uhusiano kati ya utabiri wa hali ya hewa na maamuzi yanayofanyika katika ngazi mbalimbali, ili taarifa za hali ya hewa zisitumike tu kueleza kitakachotokea, bali ziwe msingi wa hatua zinazoweza kupunguza madhara kwa wananchi, mali na shughuli za kiuchumi.

Programu hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), Taasisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza (UK Met Office) na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO