Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema shule mpya zaidi ya 29 za sekondari zinajengwa kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi 230,000 wanaotarajiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2028.
Akizungumza Dar es Salaam leo Septemba 17, 2026 katika kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, amesema hatua hiyo inatokana na mabadiliko ya mtaala wa elimu utakaosababisha wanafunzi wa darasa la saba wa mwaka 2027 kumaliza pamoja elimu ya msingi na wanafunzi wa darasa la sita.
“Maeneo mbalimbali kuna shule za ghorofa zinajengwa. Kwa sasa hivi uwezo wa Dar es Salaam ni kuchukua wanafunzi 91,000 wanaoanza kidato cha kwanza lakini mwaka 2028 wanafunzi watakaojiunga ni 230,000.
“Madarasa mapya yanayohitajika ni zaidi ya 2,000 katika manispaa zote. Kwa mantiki hiyo tumeweka mipango na mikakati. Halmashauri zote zimetenga bajeti ya Sh bilioni 72 kwa ujenzi wa madarasa. Pia tutajenga madarasa 700 katika halmashauri zote kwa kipindi hiki kilichopo,” amesema.
Pia amesema katika mpango huo wanakusudia kushirikiana na wamiliki wa shule binafsi.
“Kuna baadhi ya watu walijenga shule kubwa zamani kwa mfano St. Mathew, St. Mary, Tusiime, Happy Skillful, shule za wazazi Tabata, Gongo la Mboto, Green Acres, Andrew Father na nyingine. Kwa sababu ya kuboreshwa kwa shule za serikali sasa hivi majengo mengi ya shule hizo yamebaki tupu.
“Kwa hiyo mkakati wetu mwingine ni kushirikiana na wamiliki wa shule hizo tuingize wanafunzi wetu wa serikali kwa makubaliano angalau hata kwa kulipa kodi kwa miaka minne wakati serikali inajipanga kumaliza kabisa tatizo hilo,” amesema.
Kwa upande wa serikali, amesema Rais Samia Suluhu Hassan atatoa vibali vya kuajiri walimu wapya watakaokidhi mahitaji ya wanafunzi hao.







