Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Wakati Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kikielekea kupata uongozi mpya, Serikali imewataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa chama hicho kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa amani, utulivu na kwa kuzingatia Katiba, huku viongozi watakaochaguliwa wakitakiwa kutanguliza utumishi badala ya kutawala.

Wito huo umetolewa leo, Septemba 17, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TALGWU jijini Dodoma.

Sangu amesema uongozi wa chama cha wafanyakazi ni dhamana inayopaswa kutumiwa kusikiliza na kushughulikia changamoto za wanachama, badala ya kuwa nafasi ya kujiona mwenye mamlaka juu ya wanaoongozwa.

Akirejea maandiko ya Biblia katika Marko 10:45 na Mathayo 20:26-27, Waziri huyo amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa msingi wa uongozi ni kuwahudumia wengine.

Amesema viongozi watakaochaguliwa wanapaswa kuwa tayari kusikiliza kero za wanachama na kuzishughulikia kwa uadilifu, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda umoja na mshikamano wa TALGWU.

“Uongozi ni utumishi, si kutawala,” amesema Sangu.

Amesema uchaguzi huo haupaswi kuwa chanzo cha migawanyiko miongoni mwa wanachama, bali utumike kama fursa ya kuimarisha umoja na mshikamano wa chama.

Aidha, amewapongeza viongozi na wanachama wa TALGWU kwa kudumisha amani, utulivu na ushirikiano ndani ya chama, akieleza kuwa hali hiyo ni muhimu katika kujenga mahusiano mazuri kati ya Serikali na wafanyakazi.

Katika hatua nyingine, Sangu amesema Serikali inatambua na kuthamini haki na maslahi ya wafanyakazi, akisisitiza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ipo tayari kuendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi kupitia mfumo wa majadiliano (Social Dialogue).

Amesema mfumo huo ni muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumishi, akitaja baadhi yake kuwa ni stahiki za uhamisho, malimbikizo ya madeni na masuala mengine yanayohusu maslahi ya wafanyakazi.

Kauli hiyo imekuja wakati TALGWU ikiwasilisha mbele ya mkutano huo changamoto zinazowakabili watumishi wa Serikali za Mitaa na kuiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu huo, Kaimu Katibu Mkuu wa TALGWU, Wandiba Ngocho, amesema chama hicho kimewasilisha changamoto sita zinazohitaji hatua za Serikali kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya wafanyakazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni ucheleweshaji wa fedha za likizo, ucheleweshaji wa malipo ya posho na leseni za huduma kwa baadhi ya watumishi wa kada za afya, stahiki za uhamisho, utekelezaji wa mfumo wa PEPMIS, miundo ya utumishi na mchakato wa kubadilishiwa kada (re-categorization), pamoja na kutofanya kazi kwa ufanisi kwa baadhi ya Mabaraza ya Wafanyakazi.

Ngocho amesema baadhi ya watumishi hupokea stahiki za likizo kwa awamu au baada ya muda uliopangwa, huku akieleza kuwa hali hiyo ni miongoni mwa mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Amesema pia watumishi wanaohamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine hukumbana na ucheleweshaji wa malipo ya stahiki za uhamisho.

Kuhusu mfumo wa PEPMIS, Ngocho amesema bado kuna changamoto katika utekelezaji na matumizi yake, hivyo kuiomba Serikali kuendelea kufanya maboresho yatakayorahisisha matumizi ya mfumo huo kwa watumishi.

Ngocho amesema baadhi ya watumishi hukutana na vikwazo katika mchakato wa kubadilishiwa kada kulingana na elimu na ujuzi walioupata.

Amesema suala hilo linapaswa kuangaliwa ili kuwawezesha watumishi kutumia ipasavyo taaluma na ujuzi waliopata katika utumishi wa umma.

Aidha, TALGWU imeomba kuimarishwa kwa utendaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi katika halmashauri na taasisi, ili yaweze kutekeleza ipasavyo jukumu la kuwashirikisha wafanyakazi katika masuala yanayohusu ajira na mazingira ya kazi.

Ngocho amezipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kusikiliza na kushughulikia changamoto za wafanyakazi, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi majadiliano kati ya Serikali na wafanyakazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU, Tumaini Nyamhokya, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya chama hicho na Serikali, akisema mawasiliano ya karibu na viongozi wa Serikali yamesaidia kupunguza migogoro na kuongeza tija kwa watumishi.

Nyamhokya amemshukuru Waziri Sangu kwa kuendelea kuwa msikivu katika masuala yanayowahusu wafanyakazi, akisema ushirikiano kati ya Serikali na TALGWU ni muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumishi.

Amesema vikao mbalimbali vya chama, ikiwemo Kamati ya Utendaji na Baraza Kuu, vimefanyika kwa amani na utulivu, hali ambayo amesema imeweka mazingira mazuri kuelekea uchaguzi wa viongozi.

Ameeleza kuwa TALGWU itaendelea kushirikiana ndani ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania katika kulinda haki na maslahi ya watumishi nchini.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na viongozi na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kutoka Kenya, Somalia na Malawi, pamoja na viongozi wastaafu wa TALGWU, akiwemo Katibu Mkuu Mstaafu, Rashid Mtega.

Sangu amewataka wajumbe watakaopata dhamana ya kuongoza chama hicho na wale ambao hawatachaguliwa kuendelea kushirikiana baada ya uchaguzi, akisisitiza kuwa tofauti za uchaguzi hazipaswi kuvuruga umoja wa TALGWU.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kujenga chama chenye nguvu na mshikamano, kinachoweza kusimamia kwa ufanisi maslahi ya watumishi wa Serikali za Mitaa.