Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekamilisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Mtwara hadi Lindi–Mahumbika, pamoja na njia ya kilovolti 33 kutoka Masasi hadi Newala, miradi iliyogharimu shilingi bilioni 16.2.
Miradi hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika mikoa ya Mtwara na Lindi.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Abdallah Mitenda, amesema njia ya kilovolti 132 kutoka Mtwara hadi Lindi–Mahumbika ina urefu wa kilomita 80 na imegharimu shilingi bilioni 11.6.
Amesema njia nyingine ya kilovolti 33 kutoka Masasi hadi Newala ina urefu wa kilomita 76 na imegharimu shilingi bilioni 4.6.
“Miradi hii imesaidia kuongeza usambazaji wa umeme na kuwawezesha wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuongeza kipato,” amesema Mhandisi Mitenda.
Mfanyakazi wa ETDCO kutoka Idara ya Ufundi, Bw. Gideon Peter, amesema maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Masasi hadi Mahumbika yanaendelea.
Amesema mradi huo unatarajiwa kuimarisha uunganishaji wa mikoa ya Kusini na Gridi ya Taifa, hatua itakayoongeza uwezo wa upatikanaji na usambazaji wa umeme katika maeneo husika.
Kwa upande wao, Wananchi, akiwemo Bi. Pili Omary, wameeleza kufurahishwa na kukamilika kwa miradi hiyo, wakisema imeboresha upatikanaji wa umeme ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kuimarika kwa huduma hiyo kunatoa fursa kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, zikiwemo biashara, viwanda vidogo na huduma nyingine zinazohitaji nishati ya umeme







