Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amepokea mwaliko wa kushiriki katika dua maalum ya kuwaombea viongozi wa nchi na kuliombea Taifa kutokana na matarajio ya mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya El Niño.
Rais Dkt. Mwinyi amepokea mwaliko huo leo, tarehe 16 Septemba 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na uongozi wa Almadrasat Swifat Nabawiyatil Karimah, Msolopa Kilimani.
Dua hiyo inatarajiwa kufanyika Ijumaa, tarehe 18 Septemba 2026, ikilenga kumuomba Mwenyezi Mungu kuwalinda viongozi, Taifa na wananchi wake, pamoja na kuliepusha Taifa na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameridhia ombi la madrasa hiyo la kuongeza nafasi za Hijja kutoka tatu zilizotolewa mwaka jana hadi sita mwaka huu.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza taasisi hiyo kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za kumuombea Mwenyezi Mungu amani, ustawi na maendeleo ya nchi, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kijamii na kiroho.
Naye, Amir Mkuu wa Almadrasat Swifat Nabawiyatil Karimah, Alhaj Sheikh Muhammad Salum Muhammed, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa kupokea mwaliko huo na kukubali ombi la kuongeza nafasi za Hijja kutoka tatu hadi sita, akieleza kuwa hatua hiyo imepokelewa kwa shukrani kubwa na uongozi wa madrasa.









