Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya (Mb.), amekutana na ujumbe wa ujumbe wa Serikali na wafanyabiashara 30 waandamizi kutoka Ujerumani ulioongozwa na Waziri wa Masuala ya Shirikisho, Ulaya na Kimataifa Mhe. Manfred Pentz. Mkutano huo uliofanyika Septemba 16, 2026 katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam ulilenga kujadili fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania, Ujerumani na ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika majadiliano hayo, Waziri Manfred Pentz amebainisha kuwa Ujerumani inaona fursa kubwa za kiuchumi nchini Tanzania na katika ukanda huo, hususan kwenye maeneo ya uhamishaji wa teknolojia, ubunifu na upatikanaji wa masoko. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kutatua changamoto za kodi, sera, vikwazo visivyo vya kikodi na miundombinu ili kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake, Mhe. Millya amethibitisha utayari wa Tanzania kushirikiana na wawekezaji kutoka Ujerumani, akieleza kuwa nchi ina utulivu mkubwa wa kisiasa na fursa lukuki. Amebainisha kuwa sekta za kimkakati zinazotoa fursa hizo ni pamoja na sekta ya madini, utalii, mazingira na rasilimali za asili, ambazo zipo tayari kupokea mitaji na ushirikiano mpya.

Naye Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Annett Günther amesisitiza haja ya kuhamisha ushirikiano huo kutoka kwenye majadiliano kwenda kwenye utekelezaji wa vitendo wa miradi ya maendeleo. Ameongeza kuwa jukwaa la Invest East Africa Forum litatumika kama fursa muhimu ya kupokea na kushughulikia kwa pamoja changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji wanaoingia katika ukanda huo.

Ushirikiano kati ya pande hizo mbili unazidi kupanuka katika sekta za kisasa, ikiwemo teknolojia ya Akili Bandia (AI), kufuatia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Ujerumani na Afrika Mashariki. Mkataba huo unalenga kusaidia ujumuishaji, uwezeshaji na ukuaji wa teknolojia ya AI ili kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.