BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imepata tuzo na utambuzi tano kutokana na hatua mbalimbali ilizochukua katika kukuza ujumuishi wa huduma za fedha nchini, ikiwamo kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma hizo kati ya wanawake na wanaume.

Tuzo hizo zilitolewa katika mkutano wa kimataifa wa Alliance for Financial Inclusion (AFI), uliofanyika Septemba 1 hadi 4 mwaka huu, mjini New Delhi, India, ambapo Tanzania iliwakilishwa na BoT.

Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Meneja wa Huduma Jumuishi za Fedha wa BoT, Nangi Massawe, alisema utambuzi huo umetokana na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha.

Alisema miongoni mwa tuzo hizo ni Maya Declaration Award, iliyotolewa kwa kutambua utekelezaji wa ahadi zilizowekwa na Tanzania katika kuendeleza ujumuishi wa huduma za fedha.

Massawe alisema Tanzania iliweka ahadi 15 na hadi sasa imetekeleza sita, ikiwamo kuandaa na kutekeleza mkakati wa huduma jumuishi za fedha.

Alisema Tanzania kwa sasa inatekeleza mkakati wa tatu wa ujumuishi wa huduma za fedha wa mwaka 2023–2028, baada ya mikakati ya mwaka 2013 na 2017.

Kwa mujibu wa Massawe, kiwango cha ujumuishi wa huduma za fedha nchini kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 76 mwaka 2023, huku vipimo vya kati vikionyesha kuwa kiwango hicho kimefikia karibu asilimia 80.

Alisema idadi ya watu wazima wasiokuwa na huduma rasmi za kifedha imepungua kutoka milioni 7.8 mwaka 2017 hadi milioni 6.4 mwaka 2022.

Aidha, upatikanaji wa huduma za fedha ndani ya umbali wa kilomita tano umeongezeka kutoka asilimia 86 hadi 89, huku matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu yakipanda kutoka asilimia 60 hadi 72.

Massawe alisema BoT pia imefanikiwa kupunguza pengo la kijinsia katika upatikanaji wa huduma za fedha kutoka asilimia 10 mwaka 2017 hadi asilimia 3.6, huku vipimo vya kati vikionyesha kuwa pengo hilo linaelekea kufikia asilimia mbili.

Alisema tuzo nyingine ilitolewa kutambua sera za Tanzania zinazozingatia mahitaji ya wanawake, ikiwamo kuwekwa kwa kipengele cha jinsia katika mkakati wa sasa wa huduma jumuishi za kifedha.

Alisema BoT pia imeandaa Gender Finance Framework, inayolenga kuhakikisha bidhaa na huduma za kifedha zinazingatia mahitaji halisi ya wanawake.

Massawe alisema taasisi hiyo imeendelea kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa huduma za fedha kupitia matumizi ya simu na mawakala, pamoja na kurahisisha baadhi ya mahitaji ya nyaraka za utambulisho.

Aliongeza kuwa BoT imeweka miongozo ya wakopeshaji wa kidijitali, udhibiti na uwazi wa gharama za mikopo, huku ikishughulikia changamoto ya dhamana kwa wananchi wanaohitaji mikopo.

Tuzo nyingine iliitambua BoT kama Gender Inclusive Finance Champion Institution kutokana na utekelezaji wa Denarau Action Plan, unaolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika mfumo rasmi wa fedha.

Mbali na tuzo za taasisi, watumishi wawili wa BoT walipata Technical Leadership Awards. Meneja wa Idara ya Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Fedha, Dk Khadija Kishimba, alitambuliwa katika eneo la mwenendo wa masoko na uwezeshaji wa watumiaji wa huduma za kifedha, huku Massawe akitambuliwa kwa uongozi wa sera za huduma jumuishi za kifedha.

Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Kitengo cha Elimu ya Fedha na Mwenendo wa Masoko, Violeth Luhanjo, alisema BoT imekuwa ikitumia mfumo wa kuwafundisha waelimishaji wa elimu ya fedha ambao baadaye huwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali.

Alisema hadi sasa vyuo tisa vimehusishwa katika mpango huo, huku washiriki wanaokamilisha mafunzo ya wiki mbili wakitambuliwa kama Certified Financial Education na kusaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Naye Meneja wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa BoT, Mutashobya Mushimbusi, alisema Benki Kuu imechukua hatua kuhakikisha gharama za huduma za fedha zinawekwa wazi kwa watumiaji.

Alisema BoT imeandaa mwongozo wa gharama za huduma za fedha na kuwaelekeza watoa huduma kuwaonyesha wateja gharama wanazotakiwa kulipa wakati wa kufanya miamala kupitia programu za simu au vituo vya huduma.