Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kufanyika kwa Ijitimai na kuwasili kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali kutafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo, na kuchangia ongezeko la kipato.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 17 Septemba 2026, Ikulu, Zanzibar, alipokutana na Masheikh kutoka Bungi, Mkoa wa Kusini Unguja, waliomtembelea kwa lengo la kumualika kuhudhuria Ijitimai inayotarajiwa kuanza kesho, tarehe 18 Septemba 2026.
Amesema ongezeko la wageni watakaoshiriki katika Ijitimai hiyo litachochea shughuli mbalimbali za biashara na kutoa fursa kwa wananchi kunufaika kiuchumi na kuwepo kwa washiriki kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na viongozi wa dini katika kuhakikisha Ijitimai hiyo inafanyika katika mazingira mazuri na kufikia madhumuni yaliyokusudiwa.
Aidha, amesema Ijitimai hiyo ina nafasi muhimu katika kuimarisha elimu na mafundisho ya dini, hususan kwa vijana, kuzingatia maadili mema na kujiepusha na vitendo vinavyoathiri mwenendo na mshikamano wa jamii.
Akizungumzia mvua kubwa zinazotarajiwa kunyeesha, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza Masheikh hao kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari, kufuata maelekezo ya mamlaka husika na kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa na madhara yanayoweza kujitokeza.
Amesema viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari, kusaidiana na kuendelea kujenga mshikamano wa jamii wakati wa changamoto mbalimbali.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameeleza kufurahishwa na hatua za ujenzi wa Msikiti na Madrasa katika eneo hilo, akisema miundombinu hiyo ina umuhimu katika kuimarisha elimu ya dini na malezi bora katika jamii.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kufanyika kwa Ijitimai hiyo, ikiwemo kuimarisha miundombinu muhimu ya barabara na huduma ya umeme katika maeneo husika.
Ijitimai hiyo inatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tatu na kushirikisha wageni kutoka mataifa mbalimbali, ikiwa na shughuli za kidini zikiwemo dua maalum za kuwaombea viongozi wa nchi, kuliombea Taifa pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na hali ya mvua kubwa za El Niño.
Aidha, Ijitimai hiyo inalenga kuwakutanisha waumini kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha umoja na mshikamano, sambamba na kuendeleza elimu na mafundisho ya dini ya Kiislamu.










