Mfanyakazi wa Idara ya Habari ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Kinyagulo Tuzo, maarufu King Kinya, amefariki dunia leo, Septemba 17, 2026 baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.

Taarifa iliyotolewa Ofisi ya Rasilimali watu MCL imethibitisha kutokea kifo

cha King Kinya aliyehudumu kwa miaka 17 kama mchora katuni wa magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo.

Akizungumza na Mwananchi kaka wa marehemu, Kiondo Mjema, amesema King Kinya alianza kuugua akiwa nyumbani Tabata mwanzoni mwa Julai,2026 hali iliyomfanya kukaa ndani kwa muda kabla ya kupelekwa Morogoro.

Amesema akiwa Morogoro hali yake ilizidi kuwa mbaya na baadaye alipelekwa hospitalini, ambako alilazwa kwa takriban wiki moja kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani. “Alipotoka hospitali aliambiwa arudi tena kwa ajili ya ufuatiliaji. Juzi alirudi hospitalini baada ya kusumbuliwa na tumbo, kuharisha na kutapika, akapewa dawa na kuruhusiwa kurudi nyumbani,” amesema.

Kwa mujibu wa Kiondo, hali ya marehemu ilizidi kuwa mbaya usiku wa kuamkia jana Septemba 15, 2026, akilalamikia maumivu makali ya tumbo na kichwa pamoja na kutapika na kuharisha, ambapo alifariki dunia.

Kiondo amesema msiba upo Kimara Kona na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa Septemba 18,2026 saa 10 jioni katika makaburi ya Mwananyamala.