Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza mikakati ya kukomesha utupaji wa taka hovyo jijini humo, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu watakaokiuka utaratibu wa usafi.

Akizungumza leo Septemba 17, 2026 na wahariri kutoka vyombo vya habari jijini humo Chalamila amesema tayari wadau wamepatikana kwa ajili ya kuzalisha ‘dustbin ‘zitakazowekwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, ili kuwawezesha wananchi kutupa taka katika maeneo yaliyowekwa badala ya kuzitupa hovyo.

Aidha, amesema kutakuwa na makontena maalum katika maeneo mbalimbali, ambapo wananchi watahitajika kutenganisha taka zao kabla ya kuziweka kwenye makontena hayo.

“Uchafu Dar es Salaam marufuku. Ukikamatwa unatupa taka hovyo, usilaumu, utajuta,” amesema Chalamila, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na Serikali kulinda usafi wa jiji.

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakazi wa Dar es Salaam kuzingatia usafi na kutumia maeneo maalum yatakayotengwa kwa ajili ya utupaji wa taka, akieleza kuwa usafi wa jiji ni jukumu la kila mwananchi ambapo amesisitiza kuwa shughuli hiyo itasimamiwana mgambo na mwananchi atakayekamatwa atatozwa faini ya sh 50,000.