KATIBU Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Njombe, Gumbo Mvanda, amesisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Halmashauri za mkoa huo katika kudhibiti ubora na usalama wa chakula na vipodozi kwa ajili ya kulinda afya za wananchi.

Mvanda alitoa kauli hiyo wakati wa kikao kazi cha kutathmini utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano kati ya TBS na Halmashauri za Mkoa wa Njombe kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na kuweka mikakati ya utekelezaji kwa mwaka 2026/2027.

Alisema tathmini hiyo imebainisha hatua zilizopigwa, huku ikionyesha maeneo yanayohitaji maboresho zaidi, ikiwamo uelewa mdogo wa baadhi ya wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa usajili, viwango na usalama wa chakula na vipodozi.

Kwa mujibu wa Mvanda, changamoto nyingine ni usajili wa majengo ya biashara kutokwenda sambamba na idadi ya majengo yaliyopo kwenye kanzidata, pamoja na ukaguzi wa vipodozi katika baadhi ya Halmashauri kutofikia kiwango kinachotarajiwa.

Alisema pia kuna changamoto katika ukusanyaji na ulinganifu wa taarifa za mapato kati ya mifumo ya TBS, Halmashauri na benki, pamoja na upungufu wa nyaraka na ushahidi wa ukaguzi, ikiwamo taarifa za ukamataji na utekelezaji wa hatua za kisheria.

Mvanda alizitaka Kamati za Chakula na Vipodozi, waratibu na wakaguzi kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri kuimarisha usajili wa majengo na utoaji wa vibali, ukaguzi wa bidhaa, utekelezaji wa sheria, usimamizi wa mapato na mifumo ya taarifa na ufuatiliaji.

Alisema mafanikio ya ushirikiano huo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya ukaguzi pekee, bali kwa kuangalia iwapo wafanyabiashara wanazingatia matakwa ya usajili, bidhaa zisizo salama zinadhibitiwa na wananchi wanalindwa dhidi ya madhara ya bidhaa hafifu.

Kwa upande wake, Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, alisema baadhi ya wafanyabiashara wanaotenda kinyume cha sheria hutumia mbinu mbalimbali kukwepa udhibiti wa bidhaa, hivyo kuna umuhimu kwa wakaguzi na wadau kuendelea kujadili njia bora za kukabiliana na changamoto hizo.

Alananga alisema bidhaa zisizokidhi viwango, zikiwamo baadhi ya pombe kali na vipodozi visivyofaa, zinaweza kuhatarisha afya za wananchi, hivyo mikakati itakayowekwa katika kikao hicho inapaswa kulenga kuimarisha udhibiti na ufuatiliaji wa bidhaa hizo.

Alisisitiza kuwa ushirikiano wa TBS na Halmashauri ni muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazouzwa katika maeneo mbalimbali zinakidhi viwango na matakwa ya usalama, huku wafanyabiashara wakipata elimu na wananchi wakilindwa dhidi ya bidhaa hatarishi.