Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Tanzania imekamilisha maandalizi ya kuwa
mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM and Infra for Africa Forum)utakaofanyika tarehe 5 hadi 6 Agosti, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Agosti 4, 2026 jijini Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa Mkutano huo wa kimataifa unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,200 kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika, wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa taasisi za fedha za kimataifa, wanahisa wa Africa50, wawekezaji, viongozi wa sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo.
“ Katika hafla ya ufunguzi, viongozi mbalimbali wa nchi wanatarajiwa kushiriki wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye atakuwa mwenyeji wa mkutano huu. Viongozi wengine wanaotarajiwa kushiriki ni Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Senegal, Mhe. Bassirou Diomaye Faye, na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo,” amesema Mhe. Chalamila.
Ameendelea kwa kutaja marais wengine wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria, Mhe. Bola Ahmed Tinubu, Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto pamoja na Rais wa Jamhuri ya Gabon, Mhe. Brice Clotaire Oligui Nguema.
Kwa mujibu wa Mhe. Chalamila mkutano huo unaotajwa kuwa moja ya majukwaa makubwa zaidi ya mwaka 2026 yanayolenga kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya miundombinu barani Afrika kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
Aidha, unatoa fursa adhimu kwa Tanzania kuendelea kujitangaza kama kitovu cha biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu barani Afrika.
Ametaja hatua ya Serikali kuelekea mkutano huo, kuwa itawasilisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bandari ya Dar es Salaam, miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme pamoja na miundombinu ya TEHAMA, kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kimataifa na kuharakisha utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chalamila amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mkutano huo unakuwa kielelezo cha uwezo wa Tanzania kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa na kuendeleankujenga taswira chanya ya nchi duniani.
Huku akitoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuwapokea wageni wetu kwa ukarimu, kudumisha usafi wa mazingira,kuzingatia sheria na taratibu za nchi pamoja na kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika pale utakapohitajika.
Fauka ya hayo, Mhe. Chalamila amesema kuwa Serikali inaamini mafanikio ya mkutano huo yataongeza fursa za uwekezaji, kukuza uchumi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa pamoja na kufungua ajira na fursa mpya za maendeleo kwa Watanzania.





