Rais Dk. John Magufuli kwa mara ya kwanza anatarajiwa kuvuka mipaka ya Bara la Afrika, kwa kuitembelea China kwa ziara ya kiserikali, Gazeti la JAMHURI limebaini.

China imekuwa mdau muhimu wa maendeleo wa Tanzania, kupitia mkakati mahususi wa Tanzania ya viwanda, wawekezaji kadhaa kutoka nchi hiyo ya barani Asia wameitikia wito kwa kuanzisha viwanda kadhaa hapa nchini.

Vyanzo vyetu vinasema ziara hiyo ya Rais Magufuli imekuja wakati mwafaka, ambapo China na Tanzania zinahitajiana zaidi kimkakati. Tanzania inaihitaji China katika mkakati wake wa kujenga viwanda na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

“Unajua China ni rafiki wa kweli…kuna hatua ambazo amezichukua Rais Magufuli za kuwadhibiti wanyonyaji wa rasilimali zetu zimewakera wadau wa maendeleo kutoka Bara la Ulaya.

“Ziara yake nje ya mipaka ya nchi kuanzia China, inapeleka ujumbe mzito sana, hiyo inanikumbuka miaka zaidi ya 40 iliyopita ambapo Mwalimu Julius Nyerere alikwenda China kukutana na Mwenyekiti Mao.

“Kitendo cha Rais Magufuli kuanzia huko kinaleta hisia kali zaidi, maana ni dhahiri kwamba wote tunahitajiana, China inahitaji kuwekeza viwanda vyake Afrika na Tanzania imekaa kwenye nyonga ya Afrika ambako China inaweza kunufaika zaidi,” kinasema chanzo chetu.

Baadhi ya Watanzania waishio China wameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba kitendo cha Rais Magufuli kufanya ziara nchini China kitaleta imani ya wafanyabiashara wa China, hivyo Tanzania itakuwa kwenye nafasi ya kunufaika zaidi.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa Watanzania wanaoishi jijini Beijing, Salum Khamis Hussein, amesema nchi kama Tanzania ambayo inahitaji kukua kiviwanda pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa, inahitaji kuwa karibu zaidi na China.

“Tanzania inahitaji kuwa karibu zaidi na China, maana mambo mengi yanayofanywa na Rais Magufuli tunaona dhahiri namna yanavyoyakera mataifa ya Magharibi, mshirika wa kweli wa maendeleo ya Afrika kwa sasa ni China, japo tunatakiwa kujua namna ya kushirikiana naye.

“Zipo propaganda nyingi kuhusu China, hasa kwenye miradi, tumesikia kuhusu Zambia kwamba China sasa inaendesha migodi, Kenya nako tunaambiwa China wanataka kuendesha Bandari ya Mombasa, lakini ukweli ni kwamba tunawahitaji na wao wanatuhitaji, hivyo tunahitajiana,” anasema Salum.

JAMHURI limezungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye hakutaka kuzungumzia ziara hiyo isipokuwa kusisitiza kwamba huu ni mwaka wa uwekezaji.

Waziri Kabudi alisisitiza kuhusu kauli ya Rais Magufuli katika hafla ya kufungua mwaka wa mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini (Sherry Party), kwamba, mwaka 2019 ni mwaka wa uwekezaji. Hotuba hiyo ya Rais Magufuli imechapishwa katika kurasa za katikati za gazeti hili.

Kwa kuzingatia kauli hiyo ya “mwaka 2019 ni mwaka wa uwekezaji” JAMHURI linafahamu kuwa China imekuwa katika mipango ya kuwekeza viwanda 200 hapa nchini.

“Hilo (safari ya China) siwezi kulizungumzia. Ninachoweza kusema ni kwamba, kama alivyosema Mheshimiwa Rais katika ‘Sherry Party’ huu ni mwaka wa uwekezaji. Jambo jingine ninaloweza kusema ni kuwa uhusiano na ushirikiano wetu na nchi mbalimbali ni mzuri,” amesema Waziri Kabudi ambaye ameteuliwa kuongoza wizara hiyo hivi karibuni akitokea Wizara ya Katiba na Sheria.

JAMHURI limemtafuta Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ambaye hakuwa tayari kuzungumzia ziara hiyo ya Rais Magufuli nchini China, akisisitiza kuwa suala hilo halijafika ‘mezani’ kwake, kwa hiyo si busara kulizungumzia.

Katika hali isiyo ya kawaida, hata watendaji wengine kadhaa wa serikali wamekuwa wazito kuzungumzia ziara hiyo, na miongoni mwao, wameshindwa hata kuzungumzia fursa za uwekezaji zilizopo kati ya China na Tanzania.

Safari hiyo ya Rais Magufuli nchini China itakuwa ya kwanza nje ya Bara la Afrika tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015.

Rais Magufuli ataelekea China katika wakati ambao ujazo wa biashara kati ya taifa hilo na Tanzania unatajwa kufikia dola za Marekani bilioni 4.6, takriban Sh trilioni 10.3, kwa hiyo ziara yake inatajwa kuinufaisha Tanzania kupitia sera ya mambo ya nje ya diplomasia ya uchumi.

Rais Magufuli binafsi amewahi kusikika akiisifu China kwamba imekuwa ikitoa mikopo ambayo si tu ni yenye riba nafuu, bali pia isiyo na masharti ya ‘ajabu’.

Hali ilivyo

Oktoba mwaka jana China ilisherehekea miaka 69 tangu kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, siku ambayo huadhimishwa Oktoba Mosi, kila mwaka na katika shughuli hiyo, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, aliwaeleza waandishi wa habari mambo ambayo Tanzania inajivunia kutokana na uhusiano wake na China kwa zaidi ya miongo minne, akisema miongoni mwa mambo hayo ni yale ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kwa mujibu wa balozi huyo, kihistoria China iliiunga mkono Tanzania katika harakati za ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika na Tanzania kuongoza harakati za kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kutambulika katika Umoja wa Mataifa na kuwa mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyonufaika na misaada ya China tangu miaka ya 1960, na miongoni mwa manufaa hayo ni Reli ya Uhuru (Tazara) iliyojengwa kwa mkopo usio na riba kutoka China, ukiwa ni mradi mkubwa wa kwanza kufanywa na China nje ya mipaka yake.

Alieleza kuwa Tanzania pia imekuwa ikinufaika na misaada ya China katika sekta ya elimu na afya na kwamba, kwa miaka 50 sasa China imekuwa ikituma madaktari wake kufanya kazi nchini huku maelfu ya Watanzania wakipata fursa ya mafunzo nchini China.

Balozi huyo anaamini kuwa Tanzania inaweza kunufaika zaidi na China katika maeneo mengine kadhaa yakiwamo ya utalii, kilimo na uwekezaji katika viwanda.

Takwimu zinabainisha kuwa miradi mipya isiyopungua 196 imesajiliwa nchini katika sekta za viwanda, makazi, kilimo na uvuvi, na ujazo wa kibiashara kati ya China na Tanzania ukitajwa kufika dola za Marekani bilioni 4.3 kwa mwaka.

Katika moja ya mikutano ya jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika, China ilikwisha kutangaza kutenga dola za Marekani bilioni tano kununua bidhaa kutoka Afrika, hatua ambayo inatajwa kuwa ni fursa nzuri kwa Tanzania.

Rais Xi Jinping Dar

 

Machi, 2013, Rais wa China, Xi Jinping, alifanya ziara nchini Tanzania kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Jakaya Kikwete, na mataifa haya mawili kutia saini mikataba 17 ya ushirikiano.

Mataifa haya mawili uhusiano wake umedumu kwa miaka takriban 57 sasa, tangu iliyokuwa Tanganyika na baadaye Tanzania.

Rais Xi kwa wakati huo alifika Dar es Salaam akitokea Moscow, Urusi ambako ndiko alikoanza safari yake ya kwanza katika nchi za nje tangu kuapishwa kwake rasmi kuwa Rais wa China.

Katika mikataba hiyo 17 aliyotia saini Rais Xi, masilahi mbalimbali yaliguswa, yakiwamo ya kiuchumi na utamaduni. Miongoni mwa hayo ni ujenzi wa bandari mpya Bagamoyo pamoja na mtandao wa reli wa kuunganisha na reli nyingine za Tanzania.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam kwa wakati huo, kiongozi huyo wa China alisema ziara yake ni ishara ya uhusiano mwema kati ya nchi mbili hizi, uhusiano ambao umeendelea tangu ulipoanza wakati wa Rais Julius Nyerere na Mao Zedong.

Wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa China inaitazama Afrika kama mbia muhimu katika maendeleo ya kiuchumi, ikilenga kuwekeza katika madini, nishati na miundombinu, lakini pia Afrika ni soko muhimu la bidhaa za China.

Taarifa za mwaka 2013 wakati wa ziara hiyo zilibainisha kuwa China ni taifa la pili katika uwekezaji nchini Tanzania likitanguliwa na Uingereza.

 

Magufuli na safari za nje

Mwezi Januari mwaka 2017, Rais Magufuli ambaye imekuwa nadra kwake kusafiri nje ya nchi, kwa mara ya kwanza alisafiri nje ya Afrika Mashariki, kwenda Addis Ababa nchini Ethiopia ambako alihudhuria mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuhudhuria mkutano huo tangu aingie madarakani kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano, Novemba 2015.

Akiwa Addis Ababa, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika waliohudhuria mkutano huo, ambao vilevile ulihudhuriwa na Antonio Guterres, akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).

Ni mkutano huo ambao pia ulitumiwa kumchagua mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), iliyokuwa ikiwaniwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed, mwanadiplomasia Abdoulaye Bathily kutoka Senegal, Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad, Moussa Faki Mahamat, mwanasiasa mkongwe kutoka Botswana, Pelonomi Venson-Moitoi na aliyekuwa wakati mmoja mshauri wa rais wa Equatorial Guinea, Mba Mokuy.

 

Fursa zaidi China

Gazeti la JAMHURI linafahamu kuhusu kuwapo kwa ongezeko kubwa la wafanyabiashara kutoka Tanzania kwenda China kufanya biashara mbalimbali kama nguo, vipuri vya magari na pikipiki pamoja na vifaa vya kielektroniki.

Biashara ya nguo imekuwa ikichukua nafasi kubwa, na soko la nguo za China nchini limekuwa likikua siku hadi siku, ingawa Rais Magufuli amekuwa na msimamo wa kuhakikisha pamba ya nchini inatumika kutengeneza nguo hapa Tanzania na si kuisafirisha nje ya nchi, kisha Tanzania kuagiza nguo kutoka nje.

Mji wa Guangzhou ni moja ya miji ambayo wafanyabiashara wa nguo wa Tanzania hufika kwa ajili ya kununua na kuleta bidhaa hizo nchini.

Miji mingine ambayo wafanyabiashara wa Tanzania hufika kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za kuuza nchini ni pamoja na Shenzhen.

Please follow and like us:
Pin Share