Mpita Njia ameshitushwa na taarifa za hivi karibuni kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshika nafasi ya tatu barani Afrika katika ndoa na mimba za utotoni.

Hizi si tu ni taarifa za kushitua, bali ni taarifa za aibu katika wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Tano inajielekeza katika kuhimiza elimu kwa wote, kiasi cha kuondoa malipo ya ada.

Hili ni jambo la kushangaza. Inawezekana nawe msomaji unashangaa kama alivyoshangaa Mpita Njia. Vilevile inawezekana umejiuliza, nani hasa aliyetoa taarifa hizi? Kama umejiuliza hilo, basi utambue kuwa hizi ni taarifa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Ni kwamba, kuhusu sekeseke hili linalomshangaza na kumkera Mpita Njia, mikoa ya Katavi na Tabora ndiyo vinara wa mambo haya yasiyopaswa kuwa na nafasi katika karne hii.

Haya ni mambo yaliyowekwa bayana na Mratibu wa Afya ya Uzazi kwa Vijana kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Gerald Kihwele, wiki iliyopita katika uzinduzi wa kampeni za Jukwaa la Mawasiliano ya Afya kwa Vijana (Sitetereki) uliofanyika jijini Mwanza.

“Katika Afrika, Tanzania inashika nafasi ya tatu katika ndoa na mimba za utotoni, nyingi ni shuleni na mikoa ya Katavi na Tabora inaongoza, ikiwa Katavi ni asilimia 45 na Tabora asilimia 43,” alikaririwa akisema mwakilishi huyo kutoka wizarani na kuainisha takwimu za mikoa mingine.

Kwa mfano, Mara ikiwa na asilimia 37, Shinyanga asilimia 34, Simiyu asilimia 30 na Mwanza asilimia 28. Mpita Njia anauliza, wadau wa elimu na ustawi wa jamii katika hii mikoa wamekuwa na ushirikiano wa kiwango gani na wazee wa jadi vijijini?

Tazama takwimu hizi, mwaka 1996 wastani wa mimba za utotoni nchini ulikuwa asilimia 26.1, mwaka 1999 asilimia 24.5, mwaka 2004/2005 asilimia 26, mwaka 2010 asilimia 22 na mwaka 2015/2016 asilimia 27. Sasa tafakari, mwenendo huu usio na tija kwa taifa unakomeshwa kwa namna gani?

Mpita Njia anatambua kuwa moja ya hatua za kukomesha hali hiyo ni kuendesha kampeni mahususi dhidi ya kadhia hii, lakini kampeni pekee inatosha? Bila shaka pamoja na kampeni, ni lazima nguvu za kisheria ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wahusika, kwa kuwa ni dhahiri kuwa vitendo hivi vitakuwa vinakatisha ndoto za maisha za watoto hawa.

Achilia mbali sababu zinazotajwa kuwa ni chanzo cha hali hii, ambazo ni pamoja na umaskini katika familia au huduma rafiki za afya kwa vijana, ukweli ni kwamba hatua dhidi ya wahusika wa suala hili zinapaswa kuwa kali. Kimsingi Mpita Njia anaamini kuwa katika kukabiliana na suala hili jamii inatakiwa kuunganisha nguvu zake, iwe ngazi ya familia, kitongoji ama kijiji. Tuliepushe taifa letu katika aibu hii.

Please follow and like us:
Pin Share