Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema takribani shilingi trilioni 8.64 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo itakayoimarisha uchumi wa nchi na maendeleo ya watu hadi kufikia Januari, 2023.

Majaliwa ametaja miradi hiyo saba kuwa ni ya reli, barabara, viwanja vya ndege, huduma za jamii na nishati, ambayo utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 5, 2023) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 762.99 kutekeleza mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) ambapo kipande cha Dar es Salaam – Morogoro chenye urefu wa kilomita 300 utekelezaji umefikia asilimia 97.91.

Ameendelea kusema kuwa kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) asilimia 92.23; kipande cha Mwanza – Isaka (km 341) asilimia 25.75; kipande cha Makutupora – Tabora (km 371) asilimia 4.59 na kuanza kwa ujenzi wa kipande cha Tabora – Isaka (km 165) na Tabora – Kigoma (Km 506).

Akizungumzia kuhusu mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imetoa takribani shilingi bilioni 869.93 kwa ajili utekelezaji wa mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 83.

Amesema zoezi la ujazaji maji katika bwawa hilo lilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 22 Desemba 2022, ambapo hadi kufikia Februari, 2023 kiwango cha maji kimefikia mita 134.39 kutoka usawa wa Bahari ikilinganishwa na kiwango cha mita 163 kinachohitajika ili kuanza uzalishaji.

Waziri Mkuu amesema mradi mwingine ni uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania uliogharimu takribani shilingi bilioni 20.52, ambapo shughuli zilizofanyika katika utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege tano.

Amesema kati ya hizo, ndege moja ni aina ya Boeing 767-300F ya mizigo, ndege mbili aina ya Boeing 737-9, ndege moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na ndege moja aina ya De Havilland Dash 8-Q400. Ndege nne kati ya hizo zinatarajiwa kuwasili nchini kabla ya Novemba, 2023.

“Ndege moja ya mizigo inatazamiwa kuwasili nchini hivi karibuni. Kuwasili kwa ndege hizo kutasaidia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutanua mtandao wa safari za ndani na nje ya nchi na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi kama utalii, biashara na kilimo.”

Waziri Mkuu amesema kuwa takribani shilingi bilioni 30.39 zimetolewa na Serikali ili kulipa fidia wananchi 7,486 kati ya 9,122 wanaopisha eneo la mkuza wa mradi wa ujenzi wa bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania) lenye urefu wa km 1,443

Amsema Serikali imeendelea kulipa hisa za umiliki katika Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki hadi kufikia dola za Marekani milioni 131.0 na tayari kibali cha kuanza ujenzi wa mradi huo kimetolewa Januari 2023.

Mheshimiwa Majaliwa ametaja mradi mwingine unaotekelezwa kuwa ni ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi ambapo takribani shilingi bilioni 39.84 zimetolewa ili kuendelea na ujenzi wa kiwanda ambao umefikia asilimia 75.

Waziri Mkuu amesema katika utekelezaji wa mradi huo hekta 219 zimepandwa miwa na kufanya ukubwa wa eneo lililopandwa miwa kufikia hekta 2,974 sawa na asilimia 83 ya lengo la kupanda hekta 3,600.

Amesema kuwa kiwanda hicho kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa tani 50,000 za sukari kwa mwaka pindi kitakapoanza uzalishaji na hivyo kupunguza mahitaji ya kuagiza sukari nje ya nchi.

“Takribani shilingi bilioni 93.09 zimetolewa kuendelea na ujenzi mradi wa daraja la Kigongo-Busisi ambao umefikia asilimia 63 na kukamilika kwake kutapunguza muda wa wananchi kuvuka.”

Waziri Mkuu amesema daraja hilo litakapokamilika litapunguza muda wa wananchi kutoka eneo la Kigongo – Busisi kwa takribani muda wa saa mbili hadi dakika nne kwa kutumia usafiri wa gari na dakika 10 kwa watembea kwa Miguu.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa licha ya daraja hilo kupunguza muda wa kuvuka pia litakuwa na uwezo wa kupitisha magari ya aina yote wakati wote na kubeba uzito wa hadi tani 160.

Mheshimiwa Majaliwa amesema miradi mingine ni ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya vdege, ambapo Serikali ilitoa takribani shilingi bilioni 77.23 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambapo utekelezaji umefikia asilimia 10.2.

Amesema kazi nyingine ni kukamilika kwa upanuzi wa njia ya kutua na kuruka ndege na kufungwa kwa mfumo wa kuongozea ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma; kukamilika kwa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Geita; na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya ndege vya Songea kwa asilimia 98, Iringa asilimia 42 na Musoma asilimia 43.

By Jamhuri