Na Tatu Saad,JAMHURI MEDIA

Kocha mkuu wa Klabu ya Simba SC, Robert Oliveria ameeleza kuwaheshimu wapinzani wao ‘Raja Casablanca’ kuelekea mchezo wao wa mwisho wa kundi C, Ligi ya mabingwa Afrika,utakaopigwa huko nchini Morocco.

Robertinho ameyasema haya baada ya kundi la kwanza la wachezaji wa Simba SC kuwasili salama mjini Casablanca huko Morocco, kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kundi C dhidi ya Raja Casablanca.

Robertinho amesema: “Ni jambo zuri kuuendea mchezo huu tukiwa tayari tumeshafuzu Robo Fainali kwani hii itatupunguzia presha ya mchezo, lakini hatutauchukulia kama mchezo rahisi, bali tutacheza kwa kuwaheshimu wapinzani na kusaka mabao.”

Hata hivyo Robertinho amesema anategemea kuwaona washambuliaji wake Jean Baleke na Kibu Denis kufanya vizuri zaidi ya mchezo wa awali ambao walionesha kiwango cha juu katika safu ya ushambuliaji.

“Mchezo wetu uliopita tulikuwa na uwiano mzuri kwenye nafasi ya ushambuliaji hususani Kibu Denis na Jean Baleke, natarajia kuona wanafanya vizuri zaidi kwenye mchezo huu.”

Mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Februari 18, mwaka huu, Simba SC ilipoteza dhidi ya Raja Casablanca kwa mabao 0-3

By Jamhuri