Na Tatu Saad,JAMHURI MEDIA

Matajiri kutoka Chamazi ‘Azam FC’ wahamishia nguvu na utimamu wake kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ katika msimu huu wa 2022/23.

Hii ni baada ya kupoteza matumaini ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu 2022/23, kwa kuwa chini ya kiwango katika michezo michache ya ligi kuu hali iliyowapelekea kushuka mpaka nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara.

Afisa habari wa klabu hiyo, Hasheem Ibwe amesema wamedhamiria kufanya vizuri katika kombe la shirikisho Tanzania Bara (ASFC) kwani wanatambua umuhimu wa mashindano hayo.

“Safari hii tumedhamiria kufanya kweli kwenye Kombe la Azam Sports Federation, ndio maana tulianza kupata ushindi mkubwa kwenye michezo ile ya mwanzo, ikumbukwe tuliwafunga Malimao mabao mengi,” amesema Ibwe.

Ibwe amesema wao kama Azam FC wamejipanga vizuri na wanataka kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michuano hiyo kwa kupata matokeo mazuri kwenye kila mechi.

“Timu kubwa inafanya vitu vikubwa na kupata matokeo mazuri kwenye michezo yake, hivyo nasi tunajipanga kufanya mambo makubwa kwa kupata matokeo mazuri.amesema Ibwe

Azam FC itakuwa na kibarua cha kuikabili Mtibwa Sugar, ukiwa ni mchezo wa hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam.

By Jamhuri