Na Mwandishi wetu,JAMHURI MEDIA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema
mfumo mpya wa kupima utendaji kazi wa watumishi wa umma utatumika kubaini mikoa na halmashauri ambazo
zinaongoza kukwepa jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi

kwa kuwasilisha barua kwa Katibu Mkuu UTUMISHI kuomba ufafanuzi wa masuala ambayo mikoa na halmashauri hizo zina uwezo wa kutoa ufafanuzi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo.

Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka katika
Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, kabla ya kufungua kikao kazi cha maafisa hao kilicholenga kuzitafutia
ufumbuzi changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.


Amesema, mfumo huo utawaweka kwenye kundi la kutowajibika watumishi wote watakaosababisha mikoa na halmashauri zao kukwepa jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa kusingizia kuwa masuala hayo
yanapaswa kutolewa ufanuzi na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.


Amehoji kwanini mwajiri amuandikie barua Katibu Mkuu-UTUMISHI kuomba ufafanuzi wa jambo wakati
mwajiri huyo anaye Afisa Utumishi ambaye akishirikiana vizuri na Mwanasheria, kwa kutumia nyaraka zilizopo wana
uwezo mkubwa wa kulitolea uamuzi jambo ambalo linaombwa kutolewa ufafanuzi na Katibu Mkuu-UTUMISHI.

“Maafisa Utumishi na Wanasheria mnapaswa kushirikiana katika kutoa ufafanuzi na kufanya maamuzi ya masuala ya
kiutumishi kwa mujibu wa Kanuni, Sheria, Taratibu na Miongozo ya kiutumishi iliyopo badala ya kukwepa jukumu hilo,”
Amesema Mhagama

Kwa upande wa, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa amesema, kikao kazi hicho kimelenga kuibua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za
utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake hususani wakati wa kushughulikia masuala ya kinidhamu
ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za ucheleweshaji wa mafao ya wastaafu.


Mmoja wa washiriki wa kikao kazi hicho, ambaye ni Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Alice
Lunyata amesema amejipanga kutekeleza maelekezo ya Jenista Mhagama ya kupunguza kuwasilisha maombi Ofisi ya Rais-UTUMISHI ya kupatiwa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa kuwaelekeza, kuwapatia ufafanuzi na kuwaelimisha
watumishi wa umma kuhusiana na masuala yao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa
Umma iliyopo.


Mshiriki mwingine ambaye ni Afisa Sheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Bw. Zuberi Sarahani amesema kuwa,
yeye pamoja na Wanasheria wenzie watashirikiana na Maafisa Utumishi katika kutoa tafsiri sahihi ya Sheria, Kanuni,
Taratibu na Miongozo ili kupunguza idadi ya barua za kuomba ufafanuzi.


Naye, Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Bi. Tamko Ally amesema baada ya
kupokea maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama watahakikisha wanashirikiana na Wanasheria kusoma nyaraka na kuchambua hoja zilizowasilishwa katika taaasi zao.


Kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kimehudhuriwa na
Maafisa Utumishi na Wanasheria kutoa Sekretarieti za Mikoa 16 na Halmashauri za Wilaya 84.

By Jamhuri