Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam.

Mfanyabiashara Mohammed Dewji, maarufu ‘Mo’, amesema mazingira rafiki yaliyowekwa na Rais Samia Suluhu Hassan yamechochea maendeleo ya viwanda na kuchochea biashara


Mo pia ameshinda tuzo ya Afrika ya mzalishaji bora wa bidhaa za viwandani, iliyotolewa juzi nchini Afrika Kusini katika kilele cha tuzo za viongozi wa biashara barani Afrika (AABLA).


Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hizo Mo aliandika katika mtandao wa Twitter kuwa “Shukrani zangu ni kwa Rais Samia Suluhu kwa kujenga mazingira rafiki na chanya yanayoruhusu maendeleo ya viwanda kitaifa”
Mo ambaye ni bilionea namba moja kijana Afrika Mashariki na Kati alikabidhiwa tuzo na kiongozi wa Shirika la Maendeleo ya viwanda wa Afrika Kusini.


Katika ukurasa wa Twitter, AABLA walimpongeza Mo na kampuni anayoiongoza ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited (METL), inayofanya shughuli zake katika nchi 11 Afrika. METL inafanya biashara mchanganyiko, lakini zaidi inatengeneza nguo, unga, vinywaji na mafuta ya kupikia.


Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mo alisema kuwa amepokea tuzo hiyo kwa unyenyekevu mkubwa, huku akitoa shukurani kwa Rais Samia kwa kuweka mifumo

“Shukrani zangu ni kwa Rais Samia Suluhu kwa kujenga mazingira rafiki na chanya yanayoruhusu maendeleo ya viwanda kitaifa,” alisema Mo, ambaye hivi karibuni amenukuliwa akisema Tanzania ni salama kwa uwekezaji, kwa kuwa Serikali imeweka mifumo bora na ya wazi.


Vilevile Mo aliwapongeza washindi wote wa tuzo za AABLA na kuwasihi kuendelea kuwekeza katika kuendeleza uchumi wa bara la Afrika.
Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Mo ambaye ana miaka 48 ni tajiri namba 13 barani Afrika, akiwa na utajiri wa jumla ya Dola za Marekani 1.5 bilioni, sawa na Sh3.6 trilioni.


Mwaka 2019 ndipo utajiri wa Mo ulikuwa mkubwa zaidi kuwahi kufikiwa, ambapo ulitajwa kufikia Dola bilioni 1.9 (Sh4.5 trilioni), ambapo alishika nafasi ya 14.
Mwaka 2017 Mo katika mahojiano na Forbes, alisema miongoni mwa vitu anavyojutia ni kutowekeza katika huduma za kibenki na mawasiliano ya simu.


Alisema hakuwa na mwamko wa kujiingiza katika uwekezaji wa mtandao wa mawasiliano ya simu kwa vile alihisi wananchi wengi walikuwa hawana uwezo kumudu kununua simu na kuwasiliana.


“Lakini sasa ukiangalia nchini kila mtu anamiliki simu ya mkononi, haya ndiyo mambo mawili ambayo nayajutia,” alisema Dewji, ambaye pia ni Rais wa heshima ya klabu ya Simba.

By Jamhuri