Na Mwandishi wetu JAMHURI MEDIA, Dar es Salaam

Mmoja wa wanahisa wa kampuni mashuhuri duniani ya Microsoft na akihudumu kwa miaka 14 kama Mtendaji Mkuu wa Masuala ya Teknolojia katika kampuni hiyo maarufu duniani, Dkt. Nathan Myhrvold, leo Juni 25, 2023, amekamilisha mapumziko yake ya kiutalii nchini katika Hifadhi ta Taifa za Nyerere na Ruaha na kuondoka akiwa amefurahia kuwa nchini na familia yake.

Awali Dkt. Nathan akizungumza na ugeni wa Watendaji wa Wizara ya Utalii ulioongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, Mei 9, 2023 walipokuwa nchini Marekani aliahidi kuja Tanzania kuoumzika na ametimiza ahadi hiyo.

Mwanzilishi Mweza wa Kampuni ya kiteknolojia, microsoft Nathan Myhrvold.

“Ninavutiwa sana na vivutio vya utalii vya Tanzania. Nimeshafika Serengeti na Ngorongoro huko nyuma na safari hii nimebahatika kutembelea Ruaha na Nyerere haya ni miongoni mwa maeneo mazuri sana duniani. Tumefurahia sana,” alisema Nathan kabla ya kuondoka kwa ndege yake binafsi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam leo kurejea nchini Marekani.

“Ni faraja kwamba tulipokuwa Mei kule Seattle, Marekani na kupata fursa ya kukutana naye pamoja na mipango mingine aliyokuwa nayo alishawishika kuja Tanzania tena na tumemsikia hapa mwenyewe akisema amefurahia akiwa na familia yake na leo kwa niaba ya Mhe Waziri wetu Mhe. Mohamed Mchengerwa, tumefika hapa kuwapa zawadi kidogo na kuwaaga,” alisema Dkt. Abbasi, akiwa na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Bw. Damasi Mfugale.

Dr. Nathan, pamoja na Microsoft na kampuni ya Intellectual Venture ambayo ni Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu, pia amewekeza pamoja na Bill Gates katika kampuni nyingine kubwa ya utafiti wa masuala ya Umeme salama ya TerraPower.

Anatajwa kuwa mmoja wa wanasayansi na wagunduzi wakubwa wa nyakati hizi na mmoja wa wagunduzi wa programu ya “microsoft windows,” akiwa pia ni mwandishi mwenza na Bill Gates wa kitabu mashuhuri duniani kiitwacho “The Road Ahead.”

Kupitia taasisi yake ya Intellectual Ventures, Nathan anatajwa kuwa miongoni mwa Wamarekani 3 wakubwa wanaomiliki kisheria na kuzitumia kibiashara hakimiliki zenye thamani ya mabilioni ya gunduzi mbalimbali za kisayansi.

Dkt. Nathan ambaye kwa upande mwingine pia ni mtafiti wa sayansi za vyakula na amejenga maabara maalum ya utafiti wa vyakula akiandika pia mfululizo wa vitabu viitwavyo “Modernist Cuisines: The Art and Science of Cooking,” ameeleza kufurahishwa na ladha za baadhi ya vyakula alivyokula Tanzania kama ugali, mtori na supu ya mbuzi. Ameahidi kuendelea na tafiti za vyakula vya Tanzania.

By Jamhuri