-Tume ya Madini yaeleza usimamizi wa leseni za madini na Local Content unavyowanufaisha Watanzania
-Fursa za uwekezaji zatangazwa kuanzia utafiti, uchimbaji hadi uongezaji thamani wa madini
Dar es Salaam
Serikali imesema mageuzi yanayoendelea kutekelezwa katika sekta ya madini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye mazingira bora ya uwekezaji barani Afrika, huku ikiwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, uchakataji na uongezaji thamani wa madini.
Kauli hiyo imetolewa leo, Julai 8, 2026, na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, wakati akifungua Kongamano la Madini lililofanyika katika Ukumbi wa Dome, ndani ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba.
Dkt. Kiruswa amesema maboresho ya sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa sekta ya madini yameongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa sekta binafsi, hatua zilizochochea ongezeko la uwekezaji, ajira na mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za madini mengi, ikiwemo dhahabu, almasi, tanzanite, nikeli, kinywe (graphite), nobium, madini adimu (Rare Earth Elements), pamoja na madini ya viwandani na ujenzi.
Amebainisha kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeweka msisitizo katika kuimarisha tafiti za kijiolojia kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kufungua maeneo mapya ya uwekezaji.
“Serikali haiwaaliki wawekezaji kuja kuchimba madini pekee, bali pia kuwekeza katika tafiti za kijiolojia, teknolojia za uchenjuaji, uchakataji, uongezaji thamani wa madini na viwanda vinavyotumia madini kama malighafi,” amesema Dkt. Kiruswa.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuboresha sheria na kanuni za madini ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo kupitia matumizi ya bidhaa na huduma zinazotolewa na kampuni za wazawa.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa Programu ya Mining for Brighter Tomorrow (MBT) unaendelea kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum kunufaika na fursa zinazotokana na sekta ya madini.
Dkt. Kiruswa amesema kongamano hilo linatarajiwa kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji, huku akiwakaribisha wadau kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Madini utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, kwa lengo la kuendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha uwekezaji wa madini barani Afrika.
Akitoa mada kuhusu usimamizi wa leseni na biashara ya madini, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini wa Tume ya Madini, CPA Venance Kasiki, amesema Tume inaendelea kusimamia utoaji wa leseni za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara ya madini kwa kuzingatia Sheria ya Madini, ili kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Amesema utoaji wa leseni unazingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo sifa za waombaji, usajili wa kampuni na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kupokea na kuchakata maombi.
Ameongeza kuwa wamiliki wa leseni wanawajibika kutekeleza mipango ya uchimbaji iliyoidhinishwa, kulinda mazingira, kuajiri na kuwaendeleza Watanzania, pamoja na kutekeleza wajibu wa uwajibikaji kwa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
CPA Kasiki amesema Serikali inaendelea kuimarisha utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content), zinazolenga kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika usambazaji wa bidhaa na huduma ndani ya mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Amesema fursa hizo zinajumuisha usafirishaji, ujenzi, teknolojia, huduma za ulinzi, huduma za chakula na huduma za kifedha.
Amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa leseni za madini pamoja na utekelezaji wa Kanuni za Local Content ni nguzo muhimu katika kuongeza mapato ya Serikali, kuvutia uwekezaji, kuimarisha viwanda vya uongezaji thamani na kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na rasilimali za madini.
Vilevile, amewahimiza Watanzania kutumia fursa zinazopatikana katika sekta ya madini kwa kuwekeza katika viwanda vinavyozalisha bidhaa na vifaa vinavyotumika migodini pamoja na kutoa huduma mbalimbali zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji na uongezaji thamani wa madini.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Jumanne, amesema sekta ya madini imeendelea kutoa ajira kwa maelfu ya vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi wa maeneo yenye shughuli za uchimbaji.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama ili shughuli za uchimbaji zifanyike kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo, hatua itakayochochea maendeleo endelevu ya sekta hiyo na kuongeza mchango wake kwa uchumi wa Taifa.







