





Na.Mwandishi Wetu, Morogoro
Watumishi na wasimamizi wa shughuli za ghala nchini wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuongeza ufanisi katika biashara ya mazao ya kilimo.
Wito huo umetolewa na Afisa Tawala wa Wilaya ya Morogoro, Bi. Janeth Chatta, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, alipokuwa akifunga mafunzo ya wasimamizi wa shughuli za ghala kwa msimu wa biashara wa mbaazi na dengu 2026/2027 yaliyofanyika wilayani humo.
Bi. Chatta amesema uadilifu wa watendaji wa mfumo ni msingi wa kujenga imani kwa wakulima, wanunuzi na taasisi za fedha, huku akisisitiza kuwa Mfumo huo umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuhakikisha biashara ya mazao inafanyika kwa uwazi, ubora na ushindani.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuhimiza matumizi ya Mfumo huo pamoja na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ili kuongeza thamani ya mazao, kupanua fursa za masoko yenye ushindani na kuongeza manufaa kwa wakulima.
Aidha, amewataka washiriki kutumia maarifa waliyoyapata kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kuhakikisha taarifa za mazao zinakuwa sahihi na kwa wakati.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu na Ubora wa WRRB, Bw. Mwita Thomas, amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu walizofundishwa ili kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji, pamoja na kulinda hadhi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na WRRB yamefanyika kwa siku tano na yamehudhuriwa na washiriki 103 kutoka kampuni za uendeshaji wa ghala na wadau mbalimbali wa Mfumo huo.

