Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Benki Kuu ya Tanzania (BOT Academy) kimewahimiza Watanzania, hususani wahitimu wa elimu mbalimbali na watumishi wa sekta ya fedha, kujiunga na programu zake za mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi zinazolenga kuwajengea ujuzi wa vitendo unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na sekta ya fedha.

Akizungumza leo Julai 6, 2026 Jijini Dar es Salaam katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Mitihani wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, Beatha Rwimo, amesema chuo hicho kilichopo jijini Mwanza ni kurugenzi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na kimesajiliwa na mamlaka husika za elimu ya ufundi nchini yaani NACTVET.

Amesema Chuo kinatoa mafunzo kwa mfumo wa Competence-Based Education and Training (CBET) unaowapa wanafunzi maarifa ya kinadharia na vitendo kupitia wakufunzi wenye uzoefu mkubwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania pamoja na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za sekta ya fedha.

“Kinachotutofautisha ni kwamba tunawafundisha wanafunzi kwa vitendo kwa kutumia wataalamu waliobobea katika tasnia ya benki na fedha, jambo linalowawezesha wahitimu wetu kuwa tayari kwa soko la ajira mara wanapomaliza masomo,” amesema.

Beatha amesema Chuo kinatoa Programu ya Ordinary Diploma in Banking Practice and Supervision, inayochukua miaka miwili na kufundishwa katika kampasi ya Mwanza.

Ameeleza kuwa programu hiyo inapokea wahitimu wa kidato cha sita wenye ufaulu wa Principal Pass moja na Subsidiary Pass moja, pamoja na wahitimu wa vyeti (Certificate) katika fani za Banking, Finance, Human Resource, Information Technology, Business Administration na Procurement.

Aidha, amesema chuo kinatoa programu ya Postgraduate Diploma in Banking Management, inayofundishwa katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu ya Tanzania iliyopo Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Bi. Beatha, Programu hiyo inalenga wahitimu wa shahada na Advanced Diploma kutoka fani mbalimbali ikiwemo Uhandisi, Afya, e

Elimu, TEHAMA, Biashara na Benki, huku masomo yakifanyika kuanzia saa 11 jioni hadi saa 2 usiku ili kuwawezesha watumishi kuendelea na kazi zao wakati wakisoma.

Amesema mafunzo hayo yamekuwa na matokeo chanya kwa wahitimu wengi, ambapo baadhi yao wamepandishwa vyeo, wengine wamehamia katika nafasi za kazi za sekta ya benki na fedha, huku wamiliki wa taasisi ndogo za fedha wakitumia maarifa hayo kuboresha shughuli zao za biashara.

Mbali na programu za muda mrefu, Bi. Beatha amesema Chuo kinatoa kozi mbalimbali za muda mfupi zinazodumu kwa muda wa wiki moja hadi mbili, Programu hizo zimeandaliwa kulingana na mahitaji ya wadau wa sekta ya fedha ndani na nje ya Tanzania.

Ametaja baadhi ya kozi hizo kuwa ni Trade Finance, Environmental, Social and Governance (ESG) Practices in Banking, Climate Related Financial Risks, Certified Financial Educator, Certified Microfinance Professional na Certified Credit Risk Management.

Amesema kozi hizo zimevuka mipaka ya Tanzania na sasa zinahudumia washiriki kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Kwa mwaka huu pia tunatarajia kuanzisha kozi ya ithibati iitwayo Certification in Central Banking, ambayo itaongeza fursa kwa wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaotaka kujifunza masuala ya Benki Kuu.

Bi. Beatha amewakaribisha wananchi, watumishi wa sekta ya fedha na wahitimu mbalimbali kujiunga na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania ili kupata ujuzi unaowawezesha kuongeza tija katika kazi zao na kukuza taaluma zao.