·       Yanawaandaa pia Majaji wapya kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kujiamini na kuzingatia misingi ya utoaji haki

Na HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma.

Majaji wa Mahakama ya Rufani wametakiwa kutumia mafunzo elekezi wanayopatiwa kama fursa ya kujenga uwezo, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuimarisha utoaji haki unaozingatia misingi ya Katiba, sheria na maslahi ya wananchi.

Hayo yameelezwa leo tarehe 06 Julai, 2026 na Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)-Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yanayofanyika kwenye Ukumbi wa miktano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju na yamewaleta pamoja Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani kwa lengo la kuwaandaa kuanza kutekeleza majukumu yao katika ngazi hiyo ya juu ya utoaji haki.

Akitoa salamu zake, Mhe.Dkt. Kihwelo amemshukuru Mungu kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo na Jaji Mkuu kwa kuridhia kufanyika kwa mafunzo hayo, kushiriki katika ufunguzi wake pamoja na kukubali kuwa mmoja wa Wawezeshaji wa mafunzo hayo licha ya majukumu yake mengi ya kiuongozi.

Amesema ushiriki wa Jaji Mkuu kama Mwezeshaji ni ishara ya namna ambavyo Uongozi wa Mahakama ya Tanzania unavyoweka kipaumbele katika maendeleo ya taaluma na kuwajengea uwezo Majaji ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa viwango vya juu vya weledi.

Mhe.Dkt. Kihwelo pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiamini Mahakama ya Tanzania kupitia uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Rufani, akisema kwamba, hatua hiyo imeendelea kuimarisha uwezo wa Taasisi hiyo katika utoaji haki.

Sambamba na hilo, amewapongeza Majaji tisa walioteuliwa hivi karibuni kujiunga na Mahakama ya Rufani, akiwakaribisha rasmi katika ngazi hiyo ya juu ya Mhimili wa utoaji haki na kuwahimiza kutumia mafunzo hayo kama msingi wa safari yao mpya ya utumishi.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema jukumu kuu la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ni kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama ili kuboresha utendaji wao katika utoaji haki, akibainisha kuwa, mafunzo hayo yanatekeleza Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya mwaka 2019 pamoja na Sera ya Mafunzo ya Taifa.

Ameongeza kuwa, Mahakama imeendelea kujenga utamaduni wa kuhakikisha Viongozi wote wanaoteuliwa katika nafasi mpya wanapatiwa mafunzo elekezi kabla ya kuanza rasmi majukumu yao, hatua ambayo imechangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa kazi za Mahakama.

“Dhamira yetu ni kuhakikisha kila Kiongozi anayepata nafasi mpya anaingia akiwa ameandaliwa ipasavyo ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kujiamini,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa, mafunzo hayo ni ya tano kufanyika kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani tangu programu hiyo ilipoanzishwa mwaka 2019, jambo linaloonesha dhamira ya Mahakama ya Tanzania ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu.

Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Kihwelo, washiriki watapata mafunzo kutoka kwa Wawezeshaji wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya Mahakama ya Rufani, wakiwemo Majaji Waandamizi na Wastaafu, ambao watashirikiana nao kupitia majadiliano ya kitaaluma yanayojikita katika uzoefu wa kazi za kila siku.

Amesema, mada zitakazowasilishwa zimeandaliwa mahsusi kuwasaidia Majaji hao kuelewa kwa kina majukumu yao mapya, ikiwemo misingi ya utoaji haki, masuala ya utawala wa Mahakama ya Rufani, mwenendo wa mashauri yanayosikilizwa mbele ya Jaji mmoja na yale yanayosikilizwa na jopo la Majaji, maombi ya mapitio (Revision) pamoja na tofauti za kiutendaji kati ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Aidha, Jaji Kihwelo amesisitiza kuwa, mafunzo hayo pia yatawakumbusha Majaji umuhimu wa kuzingatia lengo kuu la Mahakama ambalo ni kutenda haki kwa wananchi, akieleza kuwa masharti ya kiufundi hayapaswi kuwa sababu ya kuchelewesha au kunyima haki pale mazingira ya kisheria yanaporuhusu haki kutendeka.

“Lengo kubwa la Mahakama ni kuamua migogoro na kuhakikisha haki inapatikana kwa mujibu wa Katiba na sheria. Tunapaswa kujikita zaidi katika kutatua migogoro kuliko kushikilia masharti ya kiufundi yanayoweza kuathiri upatikanaji wa haki,” amesema.

Mbali na mada za kisheria, amesema washiriki watapata mafunzo kuhusu afya ya akili na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo, akibainisha kuwa afya njema ya Jaji ni msingi muhimu wa utoaji wa maamuzi yenye ubora.

Aidha, amesema mafunzo hayo yataendeshwa kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia, ambapo washiriki watapatiwa nyenzo zote za mafunzo kupitia mfumo wa ‘QR Code’, utakaowawezesha kupata maudhui yote ya sasa pamoja na mafunzo yaliyotolewa katika programu zilizopita kwa urahisi.

Mhe.Dkt. Kihwelo ameeleza kuwa, mfumo huo wa kidijitali unapunguza matumizi ya karatasi huku ukiwapa washiriki fursa ya kurejea nyenzo hizo wakati wowote wanapozihitaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumzia mbinu ya ufundishaji, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa mfumo wa majadiliano na kubadilishana uzoefu badala ya mihadhara ya kawaida, ili kuwawezesha washiriki kujifunza kupitia uzoefu wa vitendo kutoka kwa Majaji waliobobea katika kazi za Mahakama ya Rufani.

Alisema uzoefu wa mafunzo yaliyopita umeonesha kuwa mfumo huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuwaandaa majaji wapya na kuongeza kujiamini kwao wanapoanza kutekeleza majukumu yao.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe.Dkt. Kihwelo aliishukuru Sekretarieti ya Mahakama ya Tanzania, hususan Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, pamoja na Sekretarieti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kwa maandalizi na ushirikiano uliowezesha kufanyika kwa mafunzo hayo.

Amesema ushirikiano huo unaendelea kuimarisha juhudi za Mahakama ya Tanzania katika kujenga mfumo endelevu wa maendeleo ya kitaaluma kwa Majaji na watumishi wake, hatua inayochangia kuimarisha utoaji haki nchini.

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)-Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akitoa neno la utangulizi leo tarehe 06 Julai, 2026 wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani yanayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto wakisikiliza neno kutoka kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo leo tarehe 06 Julai, 2026 wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani.

Meza Kuu ikipongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)-Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani kwa pamoja wakiwa katika hafla ya ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 06 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani wanaopatiwa mafunzo elekezi. Katikati ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)-Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)