Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amekumbusha umuhimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, kuendelea kufundisha na kukuza utumishi wa Umma Tanzania.

Ridhiwani ameyasema hayo aliposhiriki kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yaliwahusisha viongozi waliowahi kuliongoza chuo hicho, viongozi wa taasisi zilizoshirikiana nacho kwa kipindi cha miaka 25, watumishi, wahitimu na wadau mbalimbali wa maendeleo, ambapo vyeti na tuzo za shukrani vilitolewa kwa watu na taasisi zilizotoa mchango mkubwa katika mafanikio ya chuo hicho.

Amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuandaa na kuendeleza watumishi wa umma, huku kikichangia kwa kiasi kikubwa kuboresha utoaji wa huduma serikalini kupitia mafunzo na programu mbalimbali za kujenga uwezo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika mafunzo na maendeleo ya watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali, kuimarisha uwajibikaji na kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.