Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imesema imejipanga kutumia Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi salama ya kemikali, uchunguzi wa sampuli mbalimbali na huduma zinazotolewa na maabara zake zilizoidhinishwa kimataifa.

Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira wa GCLA, Dk. Shimo Peter Shimo, alisema maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuwafikia wananchi na kuwapa uelewa kuhusu nafasi ya mamlaka hiyo katika kulinda afya ya jamii, mazingira na ubora wa bidhaa zinazotumika nchini.

Alisema GCLA ndiyo maabara ya taifa ya rufaa inayofanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali, ikiwemo zinazohusiana na uchafuzi wa mazingira, ubora wa bidhaa, pamoja na vielelezo vinavyotumika katika uchunguzi wa makosa ya jinai.

“Katika maonesho haya tunatoa elimu kuhusu namna ya kuwasilisha sampuli kwa ajili ya uchunguzi, matumizi salama ya kemikali na taratibu zinazopaswa kufuatwa na watu au taasisi zinazojihusisha na kemikali,” alisema.

Dk. Shimo alisema mamlaka hiyo imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi katika kanda mbalimbali nchini, zikiwemo Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kaskazini, Kati, Kusini, Ziwa na Mashariki, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma za maabara.

Aliongeza kuwa GCLA ina jukumu la kusimamia matumizi salama ya kemikali kwa mujibu wa sheria, pamoja na kuhakikisha maabara zote zinazofanya uchunguzi wa kemikali nchini zinafanya kazi kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotambulika kitaifa na kimataifa.

Aidha, alisema maabara zote za GCLA zimepata ithibati ya kimataifa, jambo linaloimarisha uaminifu wa matokeo ya uchunguzi yanayotolewa na mamlaka hiyo kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi.

Aliwahimiza wananchi, wafanyabiashara na wadau wengine kutembelea banda la GCLA katika Maonesho ya Sabasaba ili kujifunza zaidi kuhusu huduma za maabara, usimamizi wa kemikali na mchango wa mamlaka hiyo katika kulinda afya za wananchi na mazingira.