Na Mwandishi Wetu, JamuhuriMedia, Nyasa

Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imeendelea kuonyesha mafanikio katika usimamizi wa fedha za umma baada ya kupata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mafanikio hayo yametokana na matumizi sahihi ya rasilimali za umma, ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuzingatia sheria na kanuni za usimamizi wa fedha za Serikali.

Akizungumza wakati wa Baraza Maalum la Madiwani lililopokea taarifa ya ukaguzi, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas ameipongeza halmashauri hiyo kwa hatua iliyofikia na kuitaka kuendelea kudumisha uwajibikaji, uwazi na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

Alisisitiza kuwa pamoja na kupata hati safi, halmashauri inapaswa kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na CAG ili kufunga hoja zilizobaki na kuimarisha zaidi mifumo ya usimamizi wa fedha.

Awali akifungua kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za CAG kilichofanyika Jana katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Stewart Nombo alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya madiwani, wataalamu na watumishi wa halmashauri, huku akiahidi kuwa mapendekezo yote ya ukaguzi yatafanyiwa kazi kwa wakati.

Naye katibu tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mery Makondo aliwapongeza viongozi na watumishi wa halmashauri kwa juhudi zao, akieleza kuwa hati safi ni kielelezo cha uwajibikaji na usimamizi mzuri wa rasilimali za wananchi.

Alisema kuwa kupatikana kwa hati safi ni kielelezo tosha cha kuongeza imani kwa wananchi na wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Nyasa.

Kwa upande wake Mkaguzi wa nje Nicholaus Killinga alisema kuwa hoja nyingi zinakuwepo kwenye halmashauri zinatokana na wakuu wa idara kukaimisha ofisi kwa watumishi ambao hawana majibu yaliyojitosheleza kujibu hoja hivyo ameshauri ni vyema kipindi cha ukaguzi kinapofika wawepo wahusika na si vinginevyo.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa Khalid Khalif alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ilikuwa na hoja 28 zilizoibuliwa na CAG, ambapo hoja saba zimefungwa baada ya kujibiwa, huku hoja 21 zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji