RAIS wa Marekani, Donald Trump ameionya Iran kuwa nchi yake inajiandaa kwa usiku mwingine wa mashambulizi, saa chache tu baada ya kusema kuwa makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano yamefika mwisho.
Trump ametishia kuchukua hatua hiyo, baada ya mashambulizi ya Iran katika maeneo ya kijeshi ya Marekani kwenye mataifa ya Ghuba. ”Tuliwashambulia vibaya jana usiku. Huenda tukawashambulia tena vibaya leo usiku,” alifafanua Trump.
Akizungumza Jumatano, Trump ametishia kushambulia miundombinu ya kiraia ya Iran, ikiwemo mitambo ya kuzalishia umeme, viwanda vya kusafishia maji ya bahari, na kukitwaa Kisiwa cha Kharg pamoja na miundombinu yake ya mafuta.
Trump ambaye ameyatoa matamshi hayo akiwa mjini Ankara, Uturuki pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, amesema wanaendelea kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya Iran dhidi ya meli za kibiashara katika Mlango Bahari wa Hormuz.
Kiongozi huyo wa Marekani ameishutumu Iran kwa kurusha droni na makombora kwenye meli. Matamshi yake yanaonekana kupigia msumari kauli ya awali kwamba Mkataba wa Maelewano kati ya nchi hizo mbili umesambaratika kabisa.
Hata hivyo, mazungumzo bado yanaonekana kuendelea licha ya pande zote mbili kusababisha mazungumzo hayo kuwa magumu.


