Na Mwamvua Mwinyi, JAMHURI MEDIA Chalinze

Lishe bora ni suala muhimu kwa afya ya binadamu, na ni kichocheo cha maendeleo ndani ya jamii.

Katika sekta ya elimu ,lishe ni suala mtambuka ambalo linachagiza wadau wa elimu, wazazi,walezi na jamii ,kuchangia chakula katika shule mbalimbali sanjali na shule kuanzisha bustani za mbogamboga ikiwa ni mbinu ya kuondoa tatizo la wanafunzi kushinda bila kula wakiwa shuleni .

Halmashauri ya Chalinze na Mkuranga zilizopo Mkoani Pwani ni Halmashauri moja wapo ambazo zimetumia jicho la tatu, kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa chakula kwa wanafunzi mashuleni .

Ofisa elimu Awali na Msingi, Halmashauri ya Chalinze, Miriam Kihiyo alieleza, Halmashauri hiyo imeanzisha kilimo cha mbogamboga katika shule za awali na Msingi 12 ,lengo likiwa kusaidia lishe mashuleni ili wanafunzi waweze kusoma wakiwa na afya .

Hatua hiyo, imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utoro shuleni kwa ajili ya chakula kupatikana kwa wanafunzi.

Kihiyo alieleza, mradi wa shule bora kwa kushirikiana na Serikali unaelekeza umuhimu wa lishe mashuleni ili kujenga afya bora kwa watoto waweze kuinua ufaulu.

Alieleza, kwa kipindi hiki kifupi ,lengo hilo limefanikiwa kwani imesaidia wanafunzi kupata chakula cha kulinda mwili
na shule kujipatia kipato ,kuuza kwa wananchi wanaoishi karibu na shule hizo.

“Imesaidia sana ,wanafunzi wanakula mboga walizopanda wenyewe kwa kuboresha afya zao, ufaulu wa shule unapanda kutokana na wanafunzi wanaojifunza wakiwa wabakula na sio kushinda na njaa”Hii awali ilisababisha wanafunzi kushuka kitaaluma kwa kukaa na njaa ama wakisubiri warudi majumbani kula chakula”amesema Kihiyo.

Vilevile aliongezea, shule zinajipatia kipato kupitia mradi wa mbogamboga sanjali na wanafunzi wanapata stadi za kilimo cha mbogamboga kwa faida yao ya maisha baada ya shule.

Alielezea,Jamii pia inajifunza kilimo cha mbogamboga kupitia shule hizo.

Kihiyo alihimiza ,kuanzia sasa ulimaji wa bustani na upandaji wa miti ya matunda upewe kipaumbele na kumjengea mtoto tabia ya kulima mbogamboga , matunda tangu akiwa shuleni.

Katika hatua nyingine, Kihiyo alisema mkakati huo unaenda Sambamba na Halmashauri ya Chalinze kupitia kitengo cha Lishe kutekeleza agizo la ulaji mashuleni kwa wanafunzi wote ikiwa ni agizo kutoka Serikalini.

Kwa upande wa Mwalimu wa Afya wa shule ya Msingi Bwilingu A Mwanaasha Mbaga alishukuru Serikali kwa uanzishwaji utoaji wa Vyakula shuleni.

Alieleza ,awali walipata changamoto kwa watoto kuwa watoro na kutokuelewa darasani kwasababu ya kushinda njaa lakini mikakati iliyopo ya kulima bustani mashuleni na utoaji wa vyakula umesaidia suala la utoro kupungua kwa kiasi kikubwa.

Salma Sumaye ambae ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Bwilingu A anafurahia namna ambavyo wanapewa chakula shuleni kwani kunawasaidia kusoma wakiwa na afya .

MKURANGA..

Ofisa elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Mkuranga ,Jessy Mpangala nae alieleza, wamefanikiwa kutokomeza utoro wa kudumu na wa rejareja kwa kuwapatia watoto chakula shuleni na kuanzisha mashamba darasa ya mbogamboga na mazao ya muda mfupi na mrefu.

Jessy aliongeza kusema, Jumla ya shule 30 zinatekeleza mkakati huo na kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula shuleni na kuhudhuria masomo bila kukosa .

Akizungumza na wadau wa elimu,”:;Hivi karibuni, Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, alihamasisha elimu itolewe kuhusu lishe kwa manufaa ya watoto na vizazi vijavyo.

Alihimiza ,jamii kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi ili kupambana na changamoto ya mahudhurio ya wanafunzi shuleni, kuboresha Mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa Halmashauri kuweka kwenye bajeti fedha za ujenzi wa miundombinu.

Kunenge alisema mwanafunzi anapokosa chakula shuleni anaweza kupata madhara ikiwemo kukosa usikivu wakati wa ujifunzaji, mahudhurio hafifu yanayopelekea utoro na hata kukatisha masomo na kushuka kwa ufaulu.

Kunenge alisisitiza mkoa utasimamia utekelezaji wa mikakati inayopangwa ili kuinua kiwango Cha ufaulu na kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo.

Mradi wa shule bora ,unatekelezwa kwa msaada wa Serikali ya watu wa Uingereza “UKaid” wakishirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) ,katika mikoa Tisa ya Tanzania Bara ikiwemo Pwani, Tanga,Dodoma, Singida, Kigoma, Katavi, Simiyu, Mara na Rukwa.

By Jamhuri