Na Helena Magabe, JAMHURI MEDIA Tarime.

UKOSEFU wa ofisi za madini Wilayani Tarime ni changamoto kubwa kwa wachimbaji na wamiliki wa mashimo ya dhahabu.

Licha ya kuwa Wilaya hii imejaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na madini ya dhahabu karibia kila kata bado kuna changamoto ya ukosefu wa ofisi.

Kuna soko la dhahabu katika Halmashauuri ya Mji Tarime na Vilevile katika Halmashauuri ya Tarime Vijijini kule Nyamongo ulipo mgodi wa Barrick.

Jambo la kushangaza kwa nini Serikali haijaona umuhimu wa ofisi na badala yake ikaweka masoko hali ambayo inawapa wakati mgumu wachimbaji wanapohitaji huduma kutoka ofisi ya madini.

Dhahabu kwa sehemu kubwa iko Wilayani Tarime lakini ofisi ya madini iko Mkoani hakuna hata tawi Tarime.

Kufatia changamoto hiyo wachimbaji wa mgodi wa kibaga uliopo mtaa wa Kibaga wanalalamikia kukosa huduma kwa wakati.

Wachimbaji hao wanadai kuwa kumekuwa na ucheleweshwaji wa kufanyiwa mrahaba na maofisa wa madini hali ambayo inachangia uchumi kuyumba.

Wanasema kuwa wanahifadhi mawe ya dhahabu kwa muda mrefu wakisubilia maafisa waje kuwafanyia mrahaba ambapo walikubaliana waje kwa wiki mara mbili lakini wanachelewa kuja hata zaidi ya wiki mbili.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kebaga Erasto Dismas Nkombe amsema walikubaliana na maofisa hao kuwa kila juma tatu na jumatano wafike mgodini kufanya mrahaba lakini hawafati utaratibu huo waliowekeana.

Amesema wachimbaji wanapata wakati Mugumu wa kutunza mawe wakisubilia kufanyiwa mrahaba licha ya kuwa wako tayari kulipia mrahaba huo kwa wakati.

Uchunguzi wa JAMHURI MEDIA umebaini kuwa menejimenti ya mkurugenzi wa mgodi huo haina ushirikiano mzuri na wachimbaji pia haiwahimizi watalamu wa madini kuja kufanya mrahaba kwa wakati.

Diwani wa kata ya Kenyamanyor ulipo mgodi huo Mhe Farida Joel amesema malalamiko hayo ni ya muda mrefu licha ya kuwa walikaa kikao cha WDC na Mafisa wa madini na kukubaliana wafike mara mbili kwa wiki lakini swala hilo bado halijafanikiwa.

Amefafanua kwamba wachimbaji wote si wazawa wa Kibaga mine wanatoka sehemu mbali mbali wanahitaji wauze mawe wapate hela kwa mahitaji yao.

“Wale wachimbaji si wote wazawa wa Kebaga wanatoka sehemu mbali mbali mtu anataka hata aende na mboga nyumbani anashindwa inatakiwa mtu ukimaliza kufanya kazi uende hata na mboga nyumbani hawewezi kuuza mawe wakiuza watakamatwa wameibia Serikali ” amesema Farida

Mwenyekiti wa Halmashauuri ya Mji Tarime Daniel Komote alipohojiwa na Jamuhuri media juu ya kuwepo changamoto hiyo amesema ndio kwa mara ya kwanza anaskia habari hizo na haoni kama swala hilo ni la Halmashauuri.

JAMHURI MEDIA haikusita kumwuliza kama mgodi huo hauingizi chochote katika Halmashauuri kwa maana ya kulipa CSR amesema wao hawana CSR kama ilivyo kwa mgodi wa Nyamongo bali wanunuzi wa mchanga wa dhahabu ndio wanatozwa ushuru.

Hata hivyo JAMHURI MEDIA imefanya mahojiano na Mkuu wa Wilaya Tarime Michael Mtengele juu ya swala hilo la ucheleweshwaji mrahada alisema zipo changamoto za kibinadamu.

Amesema kuwa Afisa wa madini hawezi kuja peke yake kuna timu anataka kuambatana nayo akikosekana hata mtu mmoja kati ya timu hiyo ni lazima akwame.

Amefafanuaa kuwa kazi ni kubwa migodi ni mingi Afisa anaweza akawa yuko ‘field’ na kuna majukumu ya dharula hutakiwa kuambatana na mtu wa mapato na wengineo.

Akiendelea kuzungumza amesema Mkoa una madini na kila siku madini yanaibuka hivyo kazi ni ngumu ndio maana wanakwama kufika kwa wakati kwani hata wao wanaipenda wafike kwa wakati lakini ni Binadamu wanapata changamoto.

Mmoja wa wachimbaji wadogo amesema hali inakuwa ngumu wakichelewa kufanyiwa mrahaba kwani store zinakuwa na mawe mingi yanaweza kuvamiwa.

Mchimbaji huyu ambaye hakupenda atajwe jina lake amesea endapo hali hii ya ucheleweshwaji wa mrahaba haitafanyiwa kazi wizi wa mawe unaweza kuibuka.

Amefafanua kuwa wao huchimba mawe na kuhifadhi kwenye ofisi ya mmiliki wa shimo maafisa wakija Boss mwenyeshimo hulipa mrahaba na wao husaga mawe na kuuza kisha kuchanga fedha kwa mmiliki wa shimo

Kero hii imelipotiwa Bungeni pia na Mbunge wa Tarime Mjini Michael Kembaki na kujibiwa na Naibu Waziri wa madini Steven Kiruswa.

Wachimbaji wanaiomba Serikali kupitia Waziri wa Madini Dotto Biteko kuona umuhimu wa kujengewa ofisi za madini Tarime ili kuwafikishia huduma karibu.

By Jamhuri