Wiki iliyopita, Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) lililazimika kuutolea ufafanuzi mvutano wa mgawo wa fedha za michuano ya BancABC Super 8 kati yake na Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), kilipotishia kuziondoa timu zake. Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa fedha zote zilizotolewa na wadhamini wa michuano hiyo – BancABC – zimelipwa kila sehemu kunakohusika zikiwamo timu zote zinazoshiriki, viwanja vinavyotumika, miji inakochezwa na promosheni ya masoko iliyogharimu shilingi milioni nane.

Baada ya kulipwa huko kote, Angetile alisema TFF ilibakiwa na Sh milioni 12 ambazo zipo, hivyo akashangaa ZFA kutishia kuziondoa timu za Zanzibar – Jamhuri ya Pemba, Mtende, Zimamoto na Falcon – kama haitapewa mgawo huo ili zibaki za Tanzania Bara peke yake – Simba, Azam, Mtibwa na Polisi Morogoro. Hesabu za Angetile zinaonyesha fedha zote zimelipwa kulingana na mkataba uliofikiwa baina yake na BancABC, lakini ZFA haikupata chochote licha ya kutoa timu nne kutoka Zanzibar.

 

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa TFF aliyashangaa manung’uniko ya ZFA kwa kurejea michuano ya Kombe la Ujirani Mwema iliyoshirikisha timu sita na kufanyika hivi karibuni, tatu kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Simba ikitwaa ubingwa kwa kuifunga Azam katika fainali. Azam na Simba ni kutoka Tanzania Bara. Katika michuano hiyo iliyoandaliwa na ZFA baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga iliondolewa kwa kuingiza kikosi cha pili. Jumatano iliyopita, Angetile alisema TFF haikupewa chochote na haikulalamika.

 

Sitaki kuzungumzia mgawo huo wala tuhuma zozote ila nasema michuano hiyo katika ujumla wake imekuja kwa kukurupuka na hivyo kukosa maana iliyotarajiwa. Inasemekana kuwa sababu kubwa iliyofanya Yanga ipeleke kikosi cha pili katika michuano ya Kombe la Ujirani Mwema ni kutoona faida zake, hatua iliyosababisha itimuliwe. Haikutaka wachezaji wake wachoke kukimbizana kwa ubingwa usiokuwa na lolote hata kama ingeupata, hivyo ikaelekeza nguvu zake zote katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagema, na ikafanikiwa kutetea ubingwa wake kwa kuifunga Azam katika fainali kwa mabao 2-0.

 

Nani hafahamu umuhimu wa Kombe la Kagame nje na ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Nani hajui umuhimu wake nje na ndani ya Afrika Mashariki na Kati? Yupi hajui umuhimu wake nje na ndani ya bara hili la Afrika? Hata timu zilizokuwa dhaifu kuliko zote za Wau al Salaam ya Sudan Kusini na Ports ya Djibouti zimepata uzoefu wa mechi za kimataifa, hivyo hakuna mashaka kwamba zitafaidika kwa kiasi kikubwa kwenye ligi za ndani kila moja nchini kwake.

 

Zimeingia katika ramani ya kandanda Afrika Mashariki na Kati bila kujali kwamba zilipoteza mechi zake zote. Huo unaweza kuwa mwanzo wa kutandaza soka la hali ya juu mbele ya safari. Wachezaji wake wamepata mwanga mpya dimbani kutoka Tanzania Bara, Zanzibar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda. Wamejifunza mengi kutoka kwa wanasoka mahiri kama  Khamis Kiiza, Haruna Niyonzima, Saidi Bahanuzi, Didier Kavumbagu, Mutombo Kazadi, John Bocco, Aggrey Moris, Salum Abubakar Salum, Shomari Kapombe, Mbuyu Twite, Etekiama Taddy, Deogratius Munishi, Ali Mustapha, Juma Kaseja Juma Kaseja Juma, na kadhalika.

 

Nasema TFF imekurupuka kuanzisha michuano ya Kombe la BancABC Super 8 na ndiyo maana imekosa msisimko wowote. Ndiyo maana hata Simba imeiga ilichofanya Yanga katika Kombe la Ujirani Mwema kwa kuingiza timu yake ya pili. Kama ilivyokuwa Kombe la Ujirani Mwema lililosusiwa na Yanga, michuano ya Kombe la BancABC nayo inaonekana si muhimu. Haizinufaishi kwa uhakika timu zinazoshiriki na ndiyo maana hata mashabiki nchini hawaifuatilii kama wanavyofanya kwa Ligi Kuu, Kombe la Kagame, Kombe la CAF au Klabu Bingwa Afrika.

 

Nani atapoteza muda wake kufuatilia mechi kati ya Simba ambayo ni Klabu Bingwa ya Soka Tanzania Bara dhidi ya Mtende, kwa mfano? Ni shabiki gani makini atapoteza muda wake kwenda kushuhudia Jamhuri ya Pemba na Polisi Morogoro zikichuana iwe kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam au wa CCM Kirumba kule Mwanza? Timu yoyote makini kamwe haiwezi kuvutiwa na michuano inayoletwa kwa kukurupuka na hivyo kukosa ushindani wenye tija kwake. Kwa mfano, Simba au Azam zitafaidikaje kwa kucheza na Mtende iwe katika maandalizi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) au Klabu Bingwa ya Kandanda Tanzania Bara?

 

TFF na ZFA zinaweza kuyarejesha mashindano ya Klabu Bingwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zinaweza kufanya hivyo kwa kushirikisha timu tatu kutoka kila upande kwa kutafuta mfumo maalum na rahisi wa kuzipata, lakini utakaokubalika kwa mashabiki wa soka nchini, kuheshimika na kuleta tija kwa timu zote zinazoshiriki. Inaweza pia kuiboresha michuano ya BancABC na kuwa ya kuvutia na si kuletwa kwa kukurupuka kama safari hii. Katika hali hiyo, hata timu zinazoshiriki zitashindana kwa nguvu zao zote kutafuta ubingwa ili, pamoja na heshima, michuano hiyo pia itatumika kujenga vikosi vyake au kufanyia usajili wa wachezaji wapya kwa ajili ya misimu mipya ya ligi. Mfano ni michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

 

Mbali na kutafuta ubingwa ambao una hadhi kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati uliochukuliwa na Yanga iliyokuwa ikiutetea, lakini kuna timu ambazo pia zimeitumia michuano hiyo kusajili wachezaji wapya kwa vikosi vyake. Ni hapo, kwa mfano, ambako Simba ilibaini udhaifu wa ngome yake na kulazimika kumsajili beki mahiri wa kati kutoka APR ya Rwanda, Mbuyu Twite, huku ikidaiwa kutaka kuwatema wachezaji wake watatu kutoka nje – Mudde Mussa, Salum Kinje na Lino Masombo – walioshindwa kuthibitisha ubora wao.

 

Japokuwa Twite anadaiwa kusaini tena Klabu ya Yanga na kurudisha fedha za Simba, lakini bado mabingwa hao wa Kombe la Kagame pia wamefanya hivyo kwa kuvutiwa na beki huyo wakati wa mchuano ileile. Pamoja na kutetea ubingwa wake, Yanga pia ilitumia michuano hiyo kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kumnyakua mshambuliaji Didier Kavumbagu kutoka Atletico ya Burundi, halafu Simba nayo imeliona pengo kubwa anapokosekana mshambuliaji wake hatari raia wa Uganda, Emmanuel Okwi.

 

Michuano ya BancABC imekosa maana kwa sababu imekuja kwa mtindo wa zimamoto zaidi na kukosa msisimko. Ndiyo maana hata Simba imeingiza timu ya pili huku mashabiki wa soka nchini wakionekana kutojua chochote. Mbali na hayo katika ujumla wake wote, hatua ya TFF na ZFA kugombania mgawo wa Sh milioni 12 ambazo ni chini ya mshahara wa siku moja tu kwa baadhi ya wachezaji wa timu kama za Barcelona ya Hispania, Manchester City ya England, Anzi Makachkala ya Urusi na kadhalika ndiyo aibu zaidi kwa soka la nchi hii !

 

By Jamhuri