Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Bagamoyo

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa( 2023) ,Abdallah Shaib amehimiza wananchi kuongeza matumizi ya Nishati Mbadala (gesi) ,badala ya kutumia mkaa na kuni ambao huchochea ongezeko la ukataji miti kiholela.

Alitoa msukumo huo ,katika Mbio za Mwenge wa Uhuru Halmashauri ya Bagamoyo,wakati akipokea taarifa na kukagua shughuli za mabadiliko ya tabia nchi, hifadhi ya Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya maji -upandaji wa miti, Shule ya Sekondari Hassanal Damji, pamoja na kugawa mitungi ya gesi kwa baadhi ya mama lishe kata ya Magomeni Wilayani humo.

Kiongozi huyo aliitaka Jamii,kushirikiana na Serikali kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Shaib alisema, matumizi ya Nishati mbadala ni agenda ambayo itaokoa raslimali za misitu na kimsingi ni muokozi wa maisha yetu .

Aidha anazisisitiza, Sekretariet za Mikoa na Halmashauri za wilaya, kusimamia sheria,kanuni na miongozo inayotolewa na Serikali kuhusu uhifadhi wa Mazingira,misitu na raslimali zake, Vyanzo vya maji na maeneo tengefu.

Shaib alizitaka pia kusimamia sheria ndogo ndogo zinazotungwa na Halmashauri hizo kwa lengo la kuhifadhi Mazingira,usafi na vyanzo vya maji.

Sambamba na hayo, ziandae bajeti ndogo ambazo zitaongeza nguvu katika udhibiti wa Utunzaji wa Mazingira.

Hata hivyo alisema, kwa zaidi ya asilimia 95 matendo ya shughuli za kijamii yanapelekea kuharibu Mazingira hali ambayo inaenda kuharibu ikolojia ya viumbe hai na uchumi wa Taifa.

“Ukataji wa miti usiozingatia Utunzaji wa Mazingira,hupelekea upotevu wa bioanuai ikiwemo wanyama na mimea, ardhi kupoteza rutkwauba kupungua kwa pato la Taifa linalotokana na utalii, kupungua kwa kipato cha kaya zinazotegemea raslimali za misitu kupungua kwa raslimali zitokanazo na misitu na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi.”

Vilevile, Shaib alitaka jamii kuepuka matumizi ya taka ngumu,vifungashio vya plastic ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaharibu Mazingira.

Pia ufugaji kwa kukusanya makundi makubwa ya mifugo pamoja na uchimbaji madini holela pamoja na kuzuia uvuvi haramu.

Ofisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, James Chui alisisitiza Halmashauri zote kutekeleza maagizo ya kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka sanjali na kutoa elimu ya upandaji miti kwa jamii.

“Katika Mbio za Mwenge wa Uhuru kila mradi tunaopita tunahakikisha miti 500 inapandwa kwenye kila Halmashauri na zinatakiwa kufuata maelekezo hayo” anaeleza Chui.

Mapema Mei 16 , Mwenge wa Uhuru ulipokelewa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo ukitokea Halmashauri ya Chalinze,ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Shauri Selenda alieleza, Mwenge huo utapitia miradi Tisa yenye thamani ya sh.Bilioni 2.3.

By Jamhuri