Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma.

Mamlaka ya Udhibiti wa Unusual wa Umma (PPRA) imetambulisha rasmi mfumo wake mpya wa ununuzi wa Umma wa kielektroniki ujulikanao kama NeST ili kudhibiti ununuzi wa Umma unaozingatia uwazi.

Hayo yameelezwa leo Juni 23,2023 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo,Dk. Leonada Mwagike wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kuanza kutumika kwa mfumo huo (Nest)ambao unatarajiwa kuanza kutumika rasmi Julai Mosi Mwaka huu.

Amesema kutokana na mahitaji mapya ya teknolojia pamoja na maelekezo ya Serikali ya kuimarisha eneo la ununuzi, PPRA ilianza zoezi la kusanifu mfumo huo hali inayosaidia misingi mikuu ya kimataifa ya ununuzi kuzingatiwa.

“Mfumo huu wa NeST utakuwa mbadala wa mfumo unaotumika hivi sasa wa TANePS,unatarajiwa kutatua changamoto za kiufundi na hivyo kukidhi mahitaji ya Serikali Katika Sekta ya manunuzi,”amefanua

Amesema,hadi kufikia Juni,2023 moduli muhimu kwa ajili ya kuruhusu mfumo kuanza kutumika zimesha kamilika na kwamba moduli hizo ni za usajili wa utumiaji, huduma za bidhaa na zinazoendesha na kusimamia Mchakato wa ununuzi.

“Mpango kazi huu utahakikisha kuwa hadi kufikia mwaka 2028 ujenzi wa moduli za e-Contract,e-Auction na e-Catalogue utakuwa umekamilika, e-Contract inatarajiwa kukamilika September 2023, kukamilika Kwa moduli hizi utaiwezesha mamlaka kutumia artificial intelligence Katika ununuzi wa umma,”amesema.

Dk.Mwagike amesema kutokana na kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mfumo huo,Umma unapaswa kujua kuwa kuanzia julai 1,2023 utaanza kutumika rasmi katika michakato ya ununuzi kwa baadhi ya Taasisi za umma ambazo tayari zimepatiwa mafunzo.

Amezitaja baadhi ya Taasisi hizo kuwa ni TANROADS na TARURA ambapo zabuni kutoka Taasisi hizo zimeshaanza kutangazwa na kufafanua kuwa Taasisi nunuzi zitaendelea kupatiwa mafunzo na pindi yatakapo kamilika zitaanza kutumia mfumo wa NeST.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo(PPRA)Eliakim Maswi ameeleza kuwa mamlaka imeandaa mpango kabambe wa mafunzo ambapo hadi kufikia Oktoba 1,2023 Taasisi zote za Umma zitatakiwa kuwa zimesha patiwa mafunzo na kujisajili kuanza kutumia mfumo huo.

Amefafanua kuwa utaratibu umewekwa ili Taasisi ambazo hazijapatiwa mafunzo ziweze kuendesha ununuzi wake kwa kutumia mfumo uliopo kwa kipindi hiki cha mpito cha miezi mitatu .

“Moja ya kuwa nguzo muhimu kwenye NeST ni kuwa na uwezo wa kusajili watumiaji Kwa haraka,urahisi na kwa usahihi, watumiaji watatakiwa kujisajili na kuweka taarifa zinazotakiwa kutokana na aina ya shughuli anayopanga kuifanya kwa kutumia mfumo mara moja tu,”anasema.

Ametaja baadhi ya faida zitakazo patikana baada ya kuanza kutumika kwa mfumo wa NeST kuwa ni kuongezeka kwa uwazi na kuondoa mwingiliano wa kibinadamu na kuongeza uwajibikaji.

By Jamhuri