Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora,imezindua mikataba ya huduma kwa wateja kwa Taasisi za umma huku ikitoa maagizo kwa taasisi zote za umma nchini kuwa na mikataba ya huduma kwa wateja iliyo hai .

Waziri mwenye dhamana hiyo George Simbachawene ameeleza hayo leo Juni 23,2023,jijini Dodoma katika uzinduzi wa mikataba hiyo na kuzielekeza Taasisi za umma kujenga uelewa kwa wateja kuhusu mikataba hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,George Simbachawene,akizungumza wakati wa uzinduzi wa mikataba ya huduma kwa wateja na taasisi za umma hafla iliyofanyika leo Juni 23,2023 jijini Dodoma.

Amesema,matumizi ya mikataba hiyo yataleta mafanikio kadhaa ikiwemo kuwezesha watumishi kuongeza uwajibikaji na nidhamu kazini ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa uwazi na weledi.

“,Tumezindua mikataba ya huduma Kwa wateja,ni matarajio makubwa kwetu kuwa itasaidia kuchochea ari ya kufanya kazi kwa bidii, vile vile itaongeza watumishi wa umma kuwa na utamaduni wa utendaji kazi unaojali matokeo na tija kwa wakati na kwa maslahi mapana ya watanzania,”anasisitiza

Waziri huyo pia amesema pamoja na mafaniko hayo yapo mapungufu ambayo yamejitokeza ikiwemo kukosekana na kutohuishwa kwa mikataba ya huduma kwa wateja,uelewa mdogo wa kuhusu mikataba hiyo na usimamizi usioridhisha. .

Simbachawene amesema,”Naagiza taasisi zote za umma ziwe na mikataba ya huduma kwa wateja iliyo hai pamoja na kujenga uelewa kwa wateja kuhusu mikataba hiyo ili kusiwe na malalamiko yoyote,”anasema.

Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mikataba ya huduma kwa wateja na taasisi za umma hafla iliyofanyika leo Juni 23,2023 jijini Dodoma.

Pamoja na hayo ameeleza,”Ni Matumaini yangu kuwa kuimarika kwa matumizi ya mifumo ya utendaji kazi serikalini hususani matumizi ya mikataba ya huduma kwa wateja italeta mageuzi makubwa ya utendaji unaojali matokeo na kutakuwa na ungezeko la uwajibikaji, ufanisi katika matumizi ya rasilimali nyingine katika sekta za umma,”anasisitiza.

Amesema serikali ina jukumu la kuwezesha wananchi kupata huduma bora ikiwa ni pamoja na elimu,afya,maji ,mawasiliano ambapo ili kufanikisha jambo hilo Serikali ina sanifu na kujenga mifumo.

Naye Katibu Mkuu, Ofisi Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Juma Mkomi amesema taasisi za umma zimekuwa zikiadhimisha wiki ya utumishi wa umma ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi 23 kwa lengo la kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya nchi zao.

Amefafanua kuwa ni azma ya Serikali kuhakikisha kila taasisi inakuwa na mkataba wa huduma kwa wateja na kuutekeleza ipasavyo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa umma na kwamba katika kufanikisha hilo,ofisi yake ilitoa maelekezo kwa taasisi zote za umma kuhuisha mikataba hiyo na kuhakikisha zinakuwa hai.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale , ameeleza kuwa pamoja na juhudi zilizopo bado mikataba ya watumishi wa umma katika ofisi za Serikali ya mitaa hazijazingatiwa katika ngazi ya mikoa na mitaa hivyo Serikali inaendelea kuhamasisha kila Taasisi kufuata utaratibu.

WAZIRI wa Nchi Ofisi Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,George Simbachawene,akizindua mikataba ya huduma kwa wateja na taasisi za umma hafla iliyofanyika leo Juni 23,2023 jijini Dodoma.

By Jamhuri