Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh akizungumza jana na wananchi wakati wa kufungwa  kwa kambi ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba. Katika kambi hiyo iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali hiyo jumla ya watu 708 walipata huduma ya matibabu.
Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tulizo Shemu akizungumza jana wakati wa kufungwa kwa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya siku tano iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba. Jumla ya watu 708 ambao ni watu wazima 622 na watoto 86 walipata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo.

Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Chakechake Mhe. Musa Haji Kombo akisoma jarida la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati akisubiri kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoanpi kisiwani Pemba yaliyokuwa yanatolewa katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku tano.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari na mwenzake Nassir Hamid Hamad wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba wakimsikiliza mwananchi aliyefika jana katika Hospitali hiyo kwaajili ya kufanyiwa upimaji na matibabu ya moyo.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa Afya wa Wizara hiyo, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee na Jamhuri ya Watu wa China mara baada ya kufunga kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh akizungumza na viongozi wa Wizara hiyo, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba kabla ya kufungwa kwa  kambi ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika Kisiwani humo. 
Baadhi ya Wananchi wa Kisiwa cha Pemba waliofika jana katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kwajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh wakati akifunga kambo ya siku tano ya matibabu hayo iliyofanywa na Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee. Picha na JKCI

……..…………………..

Na Mwandishi Maalum , Pemba

 Watu 708 wamepata huduma za upimaji na matibabu ya moyo  katika kambi maalum ya matibabu iliyofanyika katika  Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba.

Kambi hiyo ya siku tano ilifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee.

Akizungumza hivi jana wakati wa ufungwaji wa kambi hiyo Dkt. Tulizo Shemu ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge alisema kati ya watu waliowapima watu wazima  walikuwa 622 na watoto 86.

Dkt. Shemu alisema katika kambi hiyo walifanya vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi kwa watu 424 na mfumo wa umeme wa moyo kwa watu 297 ambapo asilimia 61 ya watu waliofanyiwa uchunguzi walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo.

Wagonjwa 65 watu wazima 44 na watoto 22 wamepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.

“Wagonjwa tuliowatibu walikuwa na  matatizo ya shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa misuli ya moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo na kwa watoto tuliwakuta na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu kutokukaa katika mpangilio wake”, alisema Dkt. Shemu.

Dkt. Shemu ambaye ni daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya moyo alisema katika upimaji huo wamekutana na changamoto ya upatikanaji wa dawa za kiwango cha juu za kutibu shinikizo la juu la damu na kuiomba Serikali kuhakikisha dawa hizo zinakuwepo katika Hospitali hiyo kwani Hospitali hiyo ni ya rufaa na inatakiwa kuwa na dawa hizo.

“Katika Hospitali hii dawa za moyo zipo lakini dawa hizi haziko katika kiwango cha juu cha kutibu magonjwa ya moyo ikiwemo shinikizo la juu la damu, tumewaandikia wenzetu wa hapa aina ya dawa ambazo ni za kiwango cha juu  na katika Taasisi yetu tunazitumia. Tunaiomba Serikali iwezeshe kusaidia ili dawa hizi zipatikane hapa”,.

“Tunaomba wagonjwa tuliowakuta na matatizo ya moyo yanayohitaji matibabu ya kibingwa wapewe rufaa ya dharura ya kuja kutibiwa JKCI kwani wengine tumewakuta na matatizo yanayohitaji kupata matibabu ya haraka lakini kama rufaa yao itapitia katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar wanaweza kuchelewa kupata huduma na kupata madhara makubwa ikiwemo kifo”, alisema Dkt. Shemu.

Kuhusu wataalamu wa moyo waliopo katika Hospitali hiyo Dkt. Shemu alisema wataalamu wazawa ni wachache lakini kama kutakuwa na wataalamu wazawa wa kutosha itasaidia kubadilishana ujuzi  wa kazi wakati ambao kambi mbalimbali za matibabu zinafanyika na katika miaka michache ijayo wataalamu hao wataweza kufanya kazi wenyewe.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kutoa wataalamu wake na kwenda kutoa huduma za kibingwa za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa Kisiwa cha Pemba.

Mhe. Hassan alisema matibabu waliyoyapata wananchi ni ya hali ya juu kwani wametibiwa na madaktari bingwa wa moyo na kuwaagiza viongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha wagonjwa 65 waliopewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI majina yao yanamfikia kabla ya siku ya Jumanne ili wananchi hao wapate matibabu kwa wakati.

“Kazi ya uhudumu wa afya ni ya wito na ya kujitoa, ninawaomba watu mliosomea kazi hizi mzifanye kwa unyenyekevu na kujitoa bila ya kujidai huku mkitoa huduma bora kwa wagonjwa kwa kufanya hivyo mtazuia vifo vingi vinavyotokana na uzembe na wananchi watafurahia matunda ya uwekezaji yaliyofanywa na Serikali yao”,.

“Tunawashukuru viongozi wetu wakuu kwa kuwa na nia ya dhati ya kuimarisha huduma za afya nchini, tunakwenda kubadilisha mfumo mzima wa huduma za afya ikiwemo miundombinu. Inawezekana kuokoa vifo visivyo vya lazima katika Hospitali zetu, ugonjwa usiowezekana kutibiwa upatiwe rufaa kwa haraka kabla ya tatizo kuwa kubwa kila mtu awajibike ipasavyo katika nafasi yake”, alisema Mhe. Hassan.

Naye Mkuu wa Idara ya Tiba Pemba Massoud Suleiman Abdulla alisema kuwepo kwa kambi hiyo kumerahisisha upatikanaji wa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchi wa kisiwa hicho na kuwaomba wananchi pindi zinapotokea fursa za upimaji wa magonjwa mbalimbali wazichangamkie.

Massoud alisema wananchi waliokutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya kibingwa hawana uwezo wa kulipia matibabu hayo hiyo ni kutokana na maisha yao kuwa ya hali ya chini na kutokuwa na bima za afya.

“Serikali yetu ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikilipa gharama za matibabu ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya Zanzibar, ninaomba kwa wagonjwa hawa waliokutwa na shida za moyo waweze kulipiwa matibabu yao mapema wasisubiri katika foleni kwani wengine wanaweza kupoteza maisha hii ni kutokana na shida kubwa walizokutwa nazo”, alisema Massoud.

ZHU Yinjun ambaye ni daktari bingwa wa moyo kutoka Jamhuri ya Watu wa China anayefanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee alisema  kuwepo kwa kambi hiyo kumempa nafasi ya kushirikiana na madaktari wenzake kutoka JKCI, kumjadili mgonjwa na kuangalia ni namna gani anaweza kupata matibabu.

“Katika kambi hii tumetoa matibabu ya hali ya juu kwa wananchi wa Pemba, nasi madaktari wa Kichina tuliopo katika Hospitali hii tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee katika kutoa huduma bora kwa wananchi wa Pemba”, alisema ZHU.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali za Rufaa na Mikoa imekuwa ikitoa huduma za tiba mkoba zijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kufanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo hadi sasa mikoa 11 imefikiwa na huduma hiyo.

By Jamhuri