Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tundururu

WAKALA wa barabara (TANROADS)Mkoa wa Ruvuma,umepokea Sh.bilioni 2.5 kati ya Sh.bilioni 6 ilizoomba ili kurejesha miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua za masika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Hayo yamesemwa jana na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Saleh Juma,baada ya kukagua kazi ya urejeshaji wa miundombinu ya daraja la Mto maarufu la Namiungo wilayani Tunduru.

Saleh,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuidhinisha fedha hizo ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwenye maeneo yenye changamoto ili kutoa fursa kwa shughuli za usafiri na usafirishaji kuendelea kama kawaida.

Aidha amesema,licha ya mvua za masika kunyesha kwa wingi mkoa Ruvuma,lakini barabara zote zilizo chini ya TANROADS zinapitika na hakuna shughuli za kijamii zilizosimama kutokana na ubovu wa barabara.

Amesema,mwezi Machi mwaka huu daraja la Namiungo lilipata athari kubwa baada ya maji ya mvua kupita juu ya daraja na kuharibu miundombinu,hali iliyosababisha magari kupita upande mmoja.

Amesema,kazi ya kurejesha miundombinu ya daraja hilo imechelewa kukamilika kutokana na changamoto ya mvua, ambapo magari ya mkandarasi yameshindwa kufika maeneo yanakopatikana mawe na vifusi.

Hata hivyo,amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi mwishoni mwa mwezi huu ili barabara hiyo irudi kwenye hali yake na wananchi waendelee kuitumia katika shughuli zao za uzalishaji mali.

“Tunamshukuru mkandarasi kwa kazi kubwa aliyofanya hadi sasa,hata hivyo tunataka aongeze kasi ili kazi zote zilizopangwa zikamilike ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, kwa sasa hivi hali ya hewa ni nzuri na hakuna changamoto yoyote”alisema Saleh.

Mhandisi wa kampuni ya Ovans Constructions Ltd iliyopewa kazi ya matengenezo ya daraja la Namiungo Azimio Mwapongo alisema,wameshindwa kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa kutokana na mvua ambapo magari yalishindwa kufika kwenye maeneo yanapopatikana mawe na udongo.

Amehaidi kufanya kazi usiku na mchana ili waweze kukamilisha kazi mwisho wa mwezi huu na ameishukuru ofisi ya meneja wa Wakala wa barabara TANROADS mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano unaowapa.

Mkazi wa kijiji cha Namiungo Juma Daud,ameipongeza serikali kwa kuharakisha urejeshaji wa miundombinu katika daraja hilo kwani litawezesha watumiaji wake hasa wenye magari makubwa na madogo kupitia bila wasiwasi.

Ameishukuru TANROADS, kuwapa kipaumbele cha kazi wakazi wa kijiji hicho ambao wanaendelea kunufaika na miradi ya ujenzi wa barabara pindi inapotokea changamoto ya uharibifu wa miundombinu kwenye barabara kuu ya Songea-Mangaka.

By Jamhuri