Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Makatibu Muhsusi na Watunza kumbukumbu kuwa na nidhamu, uadilifu na kutunza siri  kwani ndio chachu ya maendeleo.

Amesema wanapaswa kuzingatia weledi wa taaluma zao kwa kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia miongozo na taratibu za kiutendaji.

Akizungumza leo Mei 27, 2023 katika viwanja vya Fumba Zanzibar, Rais Samia amesema kiapo walichokula kina maana kubwa na kwamba  mtu akienda kinyume na kiapo, watajuana hivyo aliwataka waishi viapo vyao.

Amesema lengo la mkutano huo ni kuwanoa na kuongeza tiba na ufanisi kwenye majukumu yao kwani wanafanya kazi kwa kutegemeana.

 “Anayekujua ndiye anayekuthamini, huenda wenzangu walipomaliza shule wakaenda nafasi za juu lakini mimi nilianza kama mtunza kumbukumbu, ni taasisi ninayoijua vizuri na ndio maana nawathamini,” amesema.

Amesema amefanya kazi kwa karibu na makatibu mahususi kwa sababu wanapotumwa kumbukumbu na nyaraka yoyote walienda kwake hivyo, anajua hali zao maofisini na kwamba ni haki yake kuwanyanyua.

Amesema mkutano huo ni wa kipekee kwa makundi hayo kupata mafunzo maalum kwa kuwa na nidhamu, uadilifu na utunzaji siri sehemu za kazi kwani ni chachu ya maendeleo kitaaluma.

Rais Samia amesema nidhamu na uadilifu vinazaa  ufanisi kwa kukamilisha kazi kwa viwango vinavyotakiwa na wakati unaotakiwa.


Rais Samia ametoa siri ya kuwataka makatibu hao na Watunza kumbukumbu kufanya mkutano wao Zanzibar kwa sababu wengi wao hawajawahi kufika na hawaifahamu vilivyo.

Aidha, amewataka waajiri kutoka sekta binafsi na umma kuwaachia makatibu mahususi na Watunza kumbukumbu kupata mafunzo kama wengine wanavyonufaika

Amesema mafunzo hayo huwasaidia kupanua wigo wa taaluma zao na kwamba ndio fursa pekee kwa kada hiyo kutoka nje ya ofisi zao na kubadilisha mazingira na kupumzika.

Kuhusu kuongezwa hadhi chuo cha utumishi wa umma Tabora, alitaka kukamilishwa kwa mitaala ili kiweze kutoa mafunzo kwa watumishi Julai mwaka huu.

Amesema wawatumishi wanapaswa kujengewa uwezo zaidi ili hata nafasi za uteuzi zinapotokea waweze kuingia kwenye teuzi hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Mwinyi, Hemed Suleiman Abdullah, Makamu wa pili wa Rais Zanzibar,  amewataka kutekeleza kazi zao kwa kuzingatia kiapo walichoweka mbele ya Rais Samia.

Amewataka pia kuhakikisha maadili ya kazi yao wanayasimamia ili kuongeza ufanisi wa serikali zao.

Wana wajibu wa kuwatunza wakati wao wakitaka watunze nyaraka na kumbukumbu za serikali wanazokabidhiwa.

Aidha amewataka viongozi wao kuwatendea haki na kutimiza wajibu wao kwao ili nao waweze kutimiza wajibu wao.

“Kuna viongozi watawatengenezea mazengwe kwa kutotaka mtimize wajibu wenu na viapo vyenu, msiogope muendelee kufanya shughuli zenu kwa kuzingatia maadili,”

Kwa upande wake, Zuhura Songambele, Mwenyekiti wa chama chama cha makatibu Mahsusi, (Tapsea), amesema katika mkutano huo wa siku nne uliowashirikisha Makatibu mahsusi na watunza kumbukumbu na nyaraka kutoka Tanzania bara na Zanzibar  mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo usalama na utunzaji siri na mbinu bora za kiutendaji.

Alisema watazingatia weledi na miiko ya kitaaluma na kuahidi kutekeleza maagizo ya kutunza siria na nyaraka za serikali na kuhakikisha wanamsadia rais katika utekelezaji wa majukumu yake kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni nidhamu, uwadilifu na utunzaji siri sehemu za kazi ni chachu ya maendeleo kitaaluma.

“Hakuna maendeleo kama hakutakua na siri,  sababu ya kuvuja kwa siri ni kunatokana na kusimamiwa na baadhi ya watu ambao hawajasomea utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka licha ya kuwepo kwa vyuo mbalimbali vinavyotoa elimu hiyo.

Naye, Devota George Mrope Mwenyekiti wa chama cha makatibu mahsusi (Trampa) ameahidi “Tunakuhadi kwamba hatutoa siri, hatutoiba wala kuuza nyaraka na yoyote atakaeenda kinyume na kiapo alichoapa atabeba msasala wake yeye mwenyewe “amesema  Mlope.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, Makatibu Mahsusi pamoja na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka kabla ya kufunga Mkutano wa Kitaaluma wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) pamoja na Menejimenti ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika Fumba Zanzibar tarehe 27 Mei, 2023
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza wakati wa mkutano wa Kitaaluma wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) pamoja na Menejimenti ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) kilichofanyika Fumba Zanzibar tarehe 27 Mei, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Pongezi na Shukrani kutoka (TAPSEA) na (TRAMPA) iliyokabidhiwa kwake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati wa mkutano wa Kitaaluma wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) pamoja na Menejimenti ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) kilichofanyika Fumba Zanzibar tarehe 27 Mei, 2023.
Baadhi ya Viongozi waliohudhuria kilele cha Mkutano Maalum wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) pamoja na Menejimenti ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika Fumba Zanzibar tarehe 27 Mei, 2023.

By Jamhuri