Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametoa salamu za Rais Samia Suluhu Hassan akivitaka vyombo mbalimbali vya habari Tanzania kufanya kazi kitaaluma bila woga, upendeleo na uonevu.

Waziri Nape ametoa salamu hizo za rais jana wakati akifungua mkutano wa 12 wa kitaaluma wa wahariri unaofanyika mkoani Morogoro.

“Rais Dkt. Samia anawasalimia sana. Ameniambia, niwaambie mfanyekazi bila woga, bila upendeleo wala uonevu huku mkizingatia taaluma,” amesema.

Amesema Rais Samia ni muumini wa haki ya kujieleza na kutoa maoni, hivyo haoni sababu ya kuminya uhuru wa habari.

“Rais alishawahi kuniambia wakati wa mchakato ya kupitia Sheria ya Habari kuwa tuhakikishe hatuingilii haki ya watu kujieleza.

“Nasi tumekuwa tukilifanya hilo, niwaombe kwa pamoja tutafsiri maono ya rais wetu, yeye nia na dhamira yake ni kuona uhuru wa habari unaleta tija kwa nchi.”

Katika mkutano huo, Waziri Nape alipewa tuzo ya heshima ikiwa ni tuzo ya kwanza ya heshima kupewa waziri wa habari tangu nchi ipate uhuru.

Waziri Nape pamoja na mambo mengine amewataka waandishi wa habari kuendelea kuandika habari za uchunguzi, ili kuibua changamoto zilizopo kwenye jamiii kusaidia Serikali kutekeleza majukumu yake.

Kuhusu madeni inayodaiwa Serikali na vyombo ya habari, Waziri Nape amesema mchakato wa kulipa madeni hayo unaendelea na Serikali inatambua madeni ya zaidi ya Sh.bilioni 18.

Awali akisoma hotuba mbele ya mgeni rasimi, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuitambua tasnia ya habari na kwa mara ya kwanza imepokea muswada wa sheria namba 12 ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016.

“Kwa kweli tunamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutufungulia njia…tangu aingie madarakani amebadilisha upepo na kuweka mazingira mazuri ya mawasiliano kati ya vyombo vya habari na Serikali,” amesema Balile.

Balile amesema pamoja na unafuu uliowekwa na Serikali bado vyombo vya habari havipo vizuri kiuchumi,hata vile vilivyofunguliwa vimeshindwa kuendesha huduma hiyo kutokana na uchumi kuwa mdogo .

Hata hivyo, Balile ameikumbusha Serikali kulipa madeni yanayodaiwa na vyombo vya habari ambayo ni zaidi ya bilioni 20, ili fedha hizo ziwasaidie kuendesha kampuni zao.

Balile ameongeza kuwa TEF imetoa tuzo kwa Waziri Nape kutokana na kutambua mchango unaotolewa na Waziri huyo pamoja na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya habari nchini.

“Haijawahi kutokea Waziri kupewa tuzo na waandishi wa habari…sana sana ni kuwepo kwa kugomea kuandikwa stori zake, lakini Waziri Nape amekuwa mfano mzuri katika kutetea na kusimamia changamoto katika sekta ya habari.

“Kwa kutambua mchango huo tumeamua kumpa tuzo hivyo anakuwa waziri wa kwanza nchini kupata tuzo tunaamini kuwa mafanaikio hayo yametokana na juhudi za Serikali katika kusimamia sekta ya habari nchini,” amesema.

By Jamhuri