Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Wadau wa habari pamoja na asasi za kiraia wametambua hatua nzuri iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hasssan ya mabadiliko ya sheria mbalimbali zinazolalamikiwa.

Hayo yamebainika kwenye kongamano la siku mbili lililioanza Machi 23,2023 lililoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Shirika la Kimataifa la Utetezi wa Haki za Kijamii la (ICNL) lililofanyika Dar es Salaam.

Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe amesema kuwa madhumuni ya kongamano hilo limelenga kujadili masuala ya uhuru wa kujieleza na changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua.

“Tumetambua nia nzuri iliyofanywa na Serikali katika masuala ya uhuru wa kujieleza lakini bado kuna changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho.

“Hata hivyo kuna mabadiliko tunayaona kwenye uhuru wa kujieleza na kuna vipengele ambavyo vinalalamikiwa ambavyo vinaminyima uhuru hivyo vipengele hivyo vinatakiwa kufanyiwa marekebisho ya sheria,” amesema.

Amesema kuwa tayari Serikali imeonyesha nia nzuri ya kufanya marekebisho ya sheria ya habari hivyo asasai za kiraia zimerishishwa na jitihada hizo ambazo manufaa yake si sekta ya habari tu bali hata kwa wananchi wote kiujumla.

Naye Jaji Mstaafu Emeritus Justice Makaramba amezishauri asasi za kiraia hapa nchini ni vyema zikatazama umuhimu wa kuwa na uendelevu zaidi ili ziweze kujiendeleza na kuisaidia jamii.

Pia ameziasa kuwa na mpango maalumu wa uongozi na si kuwa asasi yenye mtu mmoja ambaye akifa na shirika nalo hufa.

“Ni vizuri asasi zikawa na mipango endelevu ambayo itasaidia jamii na pia kuzingatia sheria kwani tunaona mtu anapokufa na shirika nalo linakufa hivyo kunapokuwa na mpango maalumu ya uongozi itasaidia kuendeleza shirika hilo,” amesema.

Makaramba pia amezishauri asasi kuwekeza ili kupata fedha za kujiendesha na kupata faida itakayokwenda kusaidia huduma za kijamii.

Naye,Mkurugenzi Mtendaji wa TAMCODE,Rose Mwalongo amesema kuwa bado kunahitaji marekebisho ya vifungu vya sheria ambazo si rafiki kwa wanahabari ambavyo sisi kama asasi za kiraia tumetambua vimekuwa vikwazo.

“Bado kuna sheria kandamizi ambazo zinahitaji utetezi na jamii inapaswa kutambua kuwa uhuru wa kujieleza haumlingi mwandishi wa habari pekee bali ni kwa kila mwananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa pia kipengele kingine ambacho kimekuwa kikimnyima haki mwandishi wa habari ni sheria ya mwaka 1967 ambayo imepitwa na wakati ambapo mwandishi wa habari anazuia kwenda kwenye magereza kufanyakazi.

“Kuna vipengele vingi ambavyo vinamnyima haki mwandishi,sasa ni miaka 56 tangu kuwepo kwa sheria hiyo magereza hivyo ipo haja ya kufanyiwa marekebisho kifungu hicho na vingine ambavyo ni kandamizi,” amesema.

Akizungumzia kuhusiana na hatua ya Serikali kuzifuta asasi 500 mwaka 2020 kwa sababu mbalimbali, amesema kuwa sheria iliyotumika kuzifuta asassi hizo inahitaji kufanyiwa marekebisho kwani imekuwa kikwazo kikubwa kwa asasi za kiraia.

“Sheria iliyotumika kuzifuta asasi hizo ni vyema sasa ikabadlishwa kwani imekuwa kikwazo kwa asasi na kurudisha nyuma maendeleo,” amesema.

By Jamhuri