Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma 

Kufuatia taharuki inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu kifo cha aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Nusura Hassan Abdalla,Tume ya haki za binadamu na utawala bora imeazimia kufanya uchunguzi  huru kubaini ukweli wa tukio hilo .

Kifo cha mwanafunzi huyo kinahusishwa na tukio la ajali ya gari iliyomhusu Naibu Waziri TAMISEMI Dkt.Festo Dugange iliyotokea jijini hapa na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi.

Akizungumza jana jijini hapa, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Methew Mwaimu amesema Tume hiyo imefikia uamuzi huo Kwa kuona taarifa kuhusu matukio hayo zinakinzana na kuichanganya jamii.

“Tumefuatilia kwa ukaribu taarifa zote zinazotolewa na vyombo vinavyo shughulikia masuala ya haki jinai na kwa kutambua hilo tume inavipa heshima vyombo hivyo ,hata hivyo kunapotokea mahaka kutoka kwa wananchi kuhusu jambo lolote linaloashiria uvunjwaji wa haki tume ina Mamlaka kuingilia Kwa mujibu wa Sheria,”amefafanua.

Jaji huyo mstaafu amefafanua kuwa tume hiyo inayo mamlaka ya kuanzia uchunguzi wake yenyewe juu ya malalamiko yanayo ashiria uvunjifu wa amani na haki za binadamu ikiwa ni Pamoja na ukiukwaji wa misingi ya utawala Bora pasipo kusubiri malalamiko.

Kwa kipindi cha wiki mbili vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii vimekuwa vikiripoti kuhusu matukio hayo mawili kwamba yanahusiana na kueleza kuwa mwanafunzi huyo anayetajwa kufariki mkoani Kilimanjaro alikufa kwenye ajali iliyomhusisha Dkt.Dugange jambo ambalo linapingwa vikali na Mamlaka husika.

Aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Nusura Hassan

By Jamhuri