Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amezindua huduma za upandikizaji uloto Katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH)huku akieleza kuwa Serikali imewekeza shilingi bilioni 2.7 kwenye  huduma hiyo kwa lengo la kuwasaidia watanzania wa hali zote.

 Amesema hayo leo Jumatano, Mei 10, 2023 wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma mara baada ya kuzindua huduma za kibingwa za upandikizaji wa uloto (Bone Marrow Transplant) hasa kwa watu wenye Seli Mundu (Sickle Cell).

Amesema Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda inakuwa ya pili baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuzindua huduma hiyo ya upandikizaji wa uloto na hivyo, kuifanya kuwa miongoni mwa hospitali chache zinazotoa huduma hiyo katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

“Kuimarika kwa huduma za kibingwa na bobezi nchini kumepunguza gharama kubwa iliyokuwa inatumiwa na Serikali ili kuwezesha Watanzania wenye uhitaji kupata huduma hizo nje ya nchi. Kwa mfano, huduma hii ya upandikizaji uloto ikitolewa katika hospitali hii, itagharimu shilingi milioni 50 hadi 55 kwa mgonjwa mmoja,” amesema.

Ameongeza kuwa Upandikizaji uloto unatoa nafuu kubwa kwa wagonjwa wa seli mundo kwani huwapunguzia kwa kiasi kikubwa maumivu na maambukizi ya mara kwa mara na wakati mwingine huwa sababu ya kupona kabisa kwa ugonjwa huu wa kudumu.

“Kutokana na nafuu hiyo, mgonjwa huweza kuishi maisha yenye ubora na kushiriki vema katika shughuli mbalimbali ikiwemo masomo”amesisitiza.

Amesema uzinduzi wa huduma hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ni ushahidi tosha wa namna ambavyo Tanzania inapiga hatua kuboresha huduma za afya.

Naye Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kila mwaka duniani kote watoto wapatao 300,000 wanazaliwa na tatizo la Seli Mundu na hapa Tanzania kila mwaka wanazaliwa watoto 11,000 ambapo kati yao watoto 6,000 wanafikiwa na huduma za kliniki.

“Watoto wanaozaliwa na tatizo la seli mundu huwa wanapata maumivu ya mara kwa mara ya viungo, wanakuwa na tatizo la kupungukiwa damu, wanakosa masomo kwa miezi mingi. Kuna mzazi amesema mwanaye alikuwa anahudhuria masomo kwa miezi mitatu tu kati ya 10 anayopaswa kuwepo shuleni,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amesema wizara hiyo inaangalia uwezekano wa kuipandisha hadhi hospitali hiyo ili iwe hospitali ya Taifa badala ya kuendelea kubakia kuwa ya kanda. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika amesema kwamba tangu Januari 19, mwaka huu hadi leo, wamefanikiwa kupandikiza uloto kwa watoto watatu na wote wanaendelea vizuri.

 “Watoto wawili wanatoka kijiji jirani cha Mapinduzi na mmoja anatoka eneo la Area D hapahapa Dodoma.”

Amesema kufanyika kwa upandikizaji wa uloto kwenye hospitali hiyo, kumeifanya Tanzania iwe miongoni mwa nchi saba zinazotoa huduma hiyo barani Afrika na kuzitaja nchi nyingine zinazotoa huduma hiyo kuwa ni Algeria, Afrika ya Kusini, Misri, Morocco, Nigeria na Tunisia.

By Jamhuri