China imetuma ujumbe wake wa ngazi za juu kwa majadiliano ya kuimarisha uhusiano na mshirika wake wa muda mrefu, Korea Kaskazini.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, Wang Huning, amefanya mazungumzo mjini Pyongyang na ofisa mkuu wa chama tawala cha Korea Kaskazini, Jo Yong Won, ikiwa ni sehemu ya ziara ya ujumbe wa China nchini humo.
Katika mkutano huo uliofanyika jana Jumatano, viongozi hao walijadili njia za kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kiutamaduni na ustawi wa jamii, huku Wang akisisitiza nia ya Beijing ya kuyatekeleza makubalianoyaliyofikiwa kati ya Rais Xi Jinping na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un.
Mazungumzo haya yanajiri wakati mataifa hayo mawili yakiadhimisha miaka 65 tangu kusainiwa kwa mkataba wao wa urafiki na ulinzi wa pamoja wa mwaka 1961, huku kukiwa na wito kutoka kwa Rais Xi wa kudumisha msimamo thabiti wa kiusalama kufuatia mivutano ya sasa ya kidunia.


