- Ukaguzi wa miundombinu wabaini hakuna changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara
- Wafanyabiashara waipongeza TANESCO kwa utatuzi wa haraka wa hitilafu
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limebaini kuwa huduma ya umeme katika Jengo la Kituo cha Mabasi cha Mwenge inaendelea kuwa ya uhakika baada ya kufanya ukaguzi wa miundombinu kufuatia taarifa zilizosambaa zikidai kuwepo kwa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika eneo hilo.
Ukaguzi uliofanywa Julai 15, 2026, ulihusisha tathmini ya miundombinu ya umeme pamoja na mazungumzo na wafanyabiashara wanaofanyia shughuli zao katika jengo hilo. Matokeo ya ukaguzi yameonesha kuwa hakuna changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kama ilivyodaiwa, huku hitilafu chache zinazojitokeza zikishughulikiwa kwa wakati.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Mhandisi Jeremiah Jahulula, amesema shirika lilichukua hatua ya kufika eneo hilo ili kujiridhisha na hali halisi ya huduma na kusikiliza maoni ya wateja.
“Tumekagua miundombinu na kuzungumza na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao hapa. Tulichobaini ni kwamba huduma ya umeme ni ya uhakika, na pale hitilafu chache zinapojitokeza, hupatiwa ufumbuzi kwa wakati ili shughuli za wananchi zisiathirike,” amesema Mhandisi Jahulula.
Ameongeza kuwa TANESCO imeendelea kuimarisha mawasiliano na wateja kupitia makundi maalumu ya WhatsApp pamoja na namba ya huduma kwa wateja 180, hatua inayorahisisha upokeaji wa taarifa za hitilafu na kuzifanyia kazi kwa haraka.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wanaofanyia shughuli zao katika jengo hilo wameeleza kuridhishwa na huduma ya umeme inayotolewa, wakisema imewawezesha kuendesha biashara zao bila usumbufu.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Bi. Latifa Tuli, anayemiliki saluni katika jengo hilo, amesema hajawahi kushuhudia changamoto ya muda mrefu ya kukatika kwa umeme inayoweza kusimamisha biashara yake.
“Biashara yangu inategemea umeme kwa kiwango kikubwa. Kwa uzoefu wangu, sijawahi kukwama kufanya kazi kutokana na kukosekana kwa umeme kwa muda mrefu. Changamoto zinapotokea na kutoa taarifa TANESCO hufika kwa haraka na kuzitatua, jambo linalotupa utulivu wa kuendelea na biashara,” amesema Bi. Latifa.
Ukaguzi huo unaendelea kudhihirisha dhamira ya TANESCO ya kusimamia ubora wa huduma zake kwa karibu, kusikiliza maoni ya wateja na kuchukua hatua kwa wakati pale changamoto zinaporipotiwa.






