Secretary of Defense Caspar W. Weinberger meets with President Mobutu of Zaire in his Pentagon office, Room 3E880.

Na Nizar K Visram

Mahakama ya Kimataifa (ICJ) iliyo Uholanzi imeihukumu Uganda kuilipa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) dola za Marekani milioni 325 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 752) kama fidia kutokana na majeshi yake kuingia DRC mwaka 1998 hadi 2003. 

Majeshi ya Uganda na ya Rwanda yaliingia DRC na kuwasaidia waasi walioupindua utawala wa dikteta Mobutu Sese Seko.  

Hukumu hii iliyotolewa Februari 9, mwaka huu imekuja zaidi ya miaka 15 baada ya mahakama hiyo kuamua kuwa majeshi ya Uganda yalipoingia DRC yalikuwa yakivunja sheria ya kimataifa kwa kusababisha hasara za mali na maisha ya wananchi wa DRC. 

DRC iliwasilisha mashitaka yake mahakamani kwa mara ya kwanza mwaka 1999 na mwaka 2005 mahakama hiyo ikapitisha hukumu yenye kurasa 119, ikisema Uganda inapaswa kuilipa DRC lakini haikusema ilipe kiasi gani. DRC ilikuwa ikidai ilipwe dola bilioni 11 lakini ICJ iliamua kuwa ni vizuri nchi hizo mbili zikae chini na kuamua kiasi cha fidia.

Waliposhindwa kufikia uamuzi ndipo mahakama ikaamua fidia ya dola milioni 325. Kati ya hizo dola milioni 225 ni kwa ajili ya vifo na majeruhi, ubakaji, utumiaji wa watoto kama wanajeshi na raia nusu milioni kupoteza makazi yao. Dola milioni 40 ni kwa ajili ya mali zilizoteketezwa na dola milioni 60 ni kwa uporaji wa maliasili kama dhahabu, almasi, koltan, misitu na wanyamapori.

Jaji Mkuu wa ICJ, Joan Donoghue, alikataa madai ya DRC kuwa raia 180,000 walikufa, akisema ushahidi umeonyesha kuwa raia waliokufa ni kati ya 10,000 na 15,000 tu. Pia alisisitiza kuwa hukumu iliyotolewa ni ya fidia, wala haina lengo la kuiadhibu Uganda.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda alisema uamuzi wa mahakama haukuwa sahihi wala si wa halali. 

Kwa upande wa pili, Christian Uteki, mwanasheria wa DRC alisema uamuzi wa ICJ ni muhimu sana kwa sababu siku za usoni haitakuwa rahisi kwa majeshi ya nchi moja kuivamia nchi nyingine. 

Hata hivyo, alisema fidia iliyoamuliwa ni ndogo sana ikilinganishwa na hasara iliyopata DRC.

Jaji Donoghue alisema DRC ilishindwa kuwasilisha ushahidi wa kuaminika, kwa hiyo mahakama ikategemea ripoti iliyoandikwa na wataalamu wa UN. 

Ripoti hiyo ilisema majeshi ya Uganda yalivamia jimbo la Ituri – mashariki mwa DRC. Ndipo wakasababisha raia kupoteza maisha, kujeruhiwa na kulazimika kuhama makazi yao. Pia ripoti inazungumzia uporaji wa madini kama koltan, dhahabu na almasi pamoja na magogo na kahawa.

Mahakama ikasema fidia inaweza ikalipwa katika muda wa miaka mitano, yaani kila mwezi wa Septemba Uganda itatakiwa ilipe dola milioni 65. Ikichelewa kulipa, Uganda italazimika kulipa riba ya asilimia sita.

Mwaka 2005, ICJ iliamua kuwa Uganda ilikuwa imehalifu sheria ya kimataifa kwa kuvamia Jimbo la Ituri (lenye ukubwa sawa na Ujerumani) na kusaidia waasi waliokuwa wakipigana na majeshi ya DRC. 

Wakati huo huo mahakama iliamua kuwa DRC nayo ilifanya kosa la kuushambulia Ubalozi wa Uganda jijini Kinshasa na kuwazuia wanadiplomasia wake. Hili ni kosa kwa mujibu wa Waraka wa Vienna kuhusu uhusiano wa kidiplomasia duniani. Kwa kosa hilo DRC pia ilitakiwa ilipe fidia kwa Uganda. 

ICJ ikaziachia DRC na Uganda zikae na kukubaliana kiasi cha fidia. Mwaka 2015, DRC ikarudi ICJ na kusema kuwa mazungumzo hayakufanikiwa, hivyo ICJ ilipaswa itoe uamuzi. 

Haishangazi kuwa mazungumzo yaligonga mwamba, kwani DRC ilikuwa ikidai Uganda ilipe zaidi ya dola bilioni 11. Uganda ikasema idadi hiyo haina mashiko na inalenga kuifilisi nchi nzima.

Hukumu ya ICJ ya 2005 ni muhimu sana kwa sababu imetilia mkazo na kusisiza sheria ya kimataifa inayokataza mataifa kusuluhisha migogoro kwa kutumia majeshi. Hii ni mara ya kwanza kesi ya aina hii kuletwa mbele ya ICJ na nchi ya Kiafrika kukutwa na hatia.   

ICJ ilikataa hoja ya Uganda kuwa ilikuwa imelazimika kuingia DRC. Uganda ilisema ilikuwa ikishambuliwa na waasi walio ndani ya DRC. 

Mahakama ilisema kama ni kweli, basi Uganda ilipaswa kulifikisha suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, cha msingi ni kuwa Uganda haikushambuliwa na DRC bali na waasi kutoka DRC.

Hapa kuna tatizo la kisheria kwani baadhi ya wachambuzi wanasema sheria ya kimataifa inatoa haki pale tu nchi inaposhambuliwa na nchi nyingine, wala si na waasi kutoka nchi ya jirani.

ICJ ilikubaliana na Uganda kuwa haikuwa sera yake au ya majeshi yake kupora maliasili ya DRC. Hata hivyo Uganda ingeweza kuzuia uporaji uliofanywa na wanajeshi na wasaidizi wao lakini haikufanya hivyo. Kwa hilo Uganda ilikuwa na hatia kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.  

Kuhusu DRC kuwadhalilisha wanadiplomasia wa Uganda Agosti 1998, mahakama ilikubali kuwa DRC ilikosa kwa mujibu wa Waraka wa Vienna. Haya yalifanyika wakati majeshi ya DRC yalipovamia Ubalozi wa Uganda jijini Kinshasa. 

Pia wanadiplomasia wa Uganda walidhalilishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ndjili. Mahakama ilisema DRC iliwajibika kuwalinda wanadiploasia wa Uganda na mali zao, lakini haikufanya hivyo.   

Ni vizuri tukajua chimbuko la mgogoro huu. Tatizo lilianza pale Juvenal Habyarimana, aliyekuwa Rais wa Rwanda alipouawa baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kuanguka mjini Kigali. 

Yakazuka mauaji ya halaiki wakati wanamgambo wa Kihutu waitwao ‘Interahamwe’ walipowaua Watutsi wapatao 800,000. Wakimbizi wa Kitutsi walio nchini Uganda wakaamua kuingia Rwanda kijeshi wakiongozwa na Jenerali Paul Kagame na wakisaidiwa na Uganda. 

Utawala mpya wa Kagame ulifaulu kuzuia mauaji na kuwadhibiti Interahamwe. Lakini wengi wao wakakimbilia DRC mashariki. Wakajipanga na kuishambulia Rwanda kutoka DRC. Wakati huo huo waliwashambulia Watutsi waishio DRC wanaojulikana kama Banyamulenge, wakisaidiwa na majeshi ya Mobutu.

Rwanda na Uganda zikaamua kuwashambulia Interehamwe ndani ya DRC. Wakati huo huo wakawasaidia wapiganaji wa Laurent-Désiré Kabila waliokuwa wakipigana na Mobutu. 

Hatimaye Mobutu akakimbia na akafia Morocco. Nafasi yake ikashikwa na Rais Laurent Kabila akisaidiwa na Rwanda na Uganda. 

Baadaye Rais Kabila akataka majeshi ya Uganda na Rwanda yaondoke. Hii haikuwa rahisi kwa sababu ingewahamasisha Interahamwe. Msuguano ukaanza na matokeo yake Kabila akauawa. Nafasi yake ikachukuliwa na mtoto wake, Joseph Kabila.  Hatimaye majeshi ya Uganda yaliyokuwako DRC yakarudi kwao  Oktoba 2001.

Nchini DRC mambo yakabadilika. Marais Mobutu, Kabila baba na Kabila mwana hawapo tena. Sasa ni awamu ya Rais Félix Tshisekedi ambaye amechagua mwelekeo tofauti katika uhusiano wa kimataifa. 

Si tu yeye ameamua kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) bali uhusiano wake na Rais Museveni unaonekana kutengemaa. Sasa majeshi ya Museveni yameingia tena Ituri (DRC), mara hii kwa kushirikiana na majeshi ya Tshisekedi.

Ni kwa sababu wote wawili wana adui mmoja naye ni  waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) ambao wana uhusianao na wanajihadi (Daesh) wa ISIS walio katika nchi za Kiislamu. 

Hawa ADF walianza mwaka 1995 wakiwa na wapiganaji kutoka Uganda na DRC. Hivyo imebidi Tshisekedi na Museveni washirikiane kupambana na ADF waliojichimbia DRC mashariki.

Swali ni iwapo ushirikiano huu wa Tshisekedi na Museveni utabadilisha hukumu iliyotolewa na ICJ?

Hii ni mahakama inayosikiliza mashitaka yanayoletwa na taifa dhidi ya taifa. Mahakama hiyo ikishatoa hukumu hakuna kukata rufaa. Uganda kwa hiyo haina njia ya kukwepa kulipa.

[email protected]

0693 555373

By Jamhuri