DODOMA

Na Javius Byarushengo 

Januari 22, 2022, jeshi la Burkina Faso lilifanya mapinduzi baridi kwa kumuondoa madarakani Roch Kabore, Rais aliyechaguliwa kidemokrasia.

Kama ilivyo ada, yanapofanyika mapindiuzi, hupingwa kila kona ya dunia huku Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ikisitisha uanachama wa Burkina Faso hadi jeshi litakaporejesha utawala wa kiraia.

Ajabu kama si mshangao, licha ya kufanyika mapinduzi hayo haramu kwa kumuondoa Rais aliyechaguliwa na wananchi kidemokrasia, bado wananchi hao hao wakaingia mitaani wakiimba na kuwashangilia wanajeshi kwa kitendo cha kumng’oa aliyekuwa mtawala wao.

Je, ni nini kimesababisha wananchi wa Burkina Faso kuwa na nyuso za bashasha mbele ya wanajeshi wafanya mapinduzi?

Kwa mujibu wa nyaraka na machapisho mbalimbali kuhusu Burkina Faso, zipo sababu mbalimbali zinazofanya raia wa taifa hilo kuona ni heri kutawaliwa kijeshi kuliko kiraia.

Mosi, inasemekana serikali iliyokuwa madarakani ilishindwa kutokomeza makundi ya kigaidi  kwa kushindwa kuliwezesha jeshi kupambana kikamilifu na makundi hayo hatari, hivyo ulinzi na usalama wa raia kubaki shakani kama si njia panda.

Ufisadi na rushwa ni tatizo kubwa Burkina Faso kwani haki huuzwa sokoni kama njugumawe! Viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza wameshindwa kutimiza majukumu yao na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka wasijue pa kukimbilia.

Viongozi kujilimbikizia mali

Ni ukweli usiopingika, Burkina Faso ni miongoni mwa mataifa maskini sana duniani. Hata hivyo, licha ya umaskini wa nchi na watu wake bado ‘kakeki kadogo ka taifa’ kamekuwa kakiangukia kwenye vitambi vya watawala wachache.

Huduma za kijamii mfano elimu na matibabu ni giza nene kwa watu wa Burkina Faso. Wanaopata elimu ni watoto wa matajiri na wa viongozi wakubwa wa kisiasa, huku watoto wa makabwela wakibaki wanaitwa watoto wa mitaani kana kwamba mitaa inabeba mimba na kuzaa. 

Matibabu ni shida na watu wengi wanapoteza uhai kwa magonjwa yanayotibika, wengine walio mafukara kabisa wanakosa hata fedha za kununua kidonge cha ‘Paracetamol’ kupunguza maumivu ya kawaida. 

Viongozi wenyewe wakiugua hata malaria ya kutibu kwa mmea wa ‘Alovera’, hukimbilia Ufaransa na mataifa mengine ya Magharibi kupata tiba bora.

Ulevi wa madaraka

Viongozi wengi wamekuwa miunguwatu wakisahau kuwa uongozi ni dhamana. Hawataki kusikiliza shida na kero za wanaowaongoza. 

Macho ya watawala yanawaona wanaotawaliwa kama ‘vikatuni’ na ‘vijisanamu’. Ni mazingira haya yanayotiririsha machozi ya wananchi na kuona ni bora kuangukia na kufia mikononi mwa wavaa buti kuliko watawala hawa wasaliti.

Matabaka ni changamoto kubwa miongoni mwa watu wa Burkina Faso kwa sababu serikali iliyokuwa madarakani ilishindwa kuwaunganisha watu wake. 

Mwenye nacho anazidi kuongezewa na asiye nacho anazidi kunyang’anywa kichache alichonacho ili akatumbukie kabisa ndani ya shimo la ‘cobra’.

Mgawanyo feki wa nyadhifa

Viongozi walioko madarakani wamekuwa wakipeana nafasi nzuri za uongozi wao kwa wao na watoto wao, hivyo kuunda uongozi wa familia fulani. 

Kinachozingatiwa hapa si uwezo wa mtu au taaluma yake bali ni mtoto wa nani. Wasomi wanaotoka katika familia zisizojulikana hawapati nafasi hata kama wana uelewa mpana na uwezo wa kuongoza.

Ukosefu wa ajira ni kizungumkuti miongoni mwa wa Burkinabe. Baadhi ya vijana licha ya kujikongoja kusoma kwa taabu na mateso kutokana na umaskini uliopindukia wa familia zao na hatimaye kupata elimu, bado wamalizapo hubaki mitaani wakizunguka na vyeti vyao.

Wakishachoka huamua kuvitundika ukutani mwa vijumba vya wazazi wao vibaki kama kumbukumbu. Inasemekana wanaopata ajira nzuri ni watoto wa viongozi. Hata kazi za hadhi ya chini kuzipata inatakiwa uwe na mtu mkubwa serikalini anayekujua na si cheti chako cha ufaulu wa juu.

Hakika mazingira haya ya Burkina Faso ndiyo taswira halisi ya mataifa mengi yanayoendelea, hususan ya Afrika. 

Mataifa haya yamekuwa yakikumbwa na kadhia za mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara na kubaki yakilaani kama kuku jike amlaanivyo mwewe kwa dua lisilo na manufaa baada ya kupokonywa kifaranga chake.

Wanajeshi waliopewa majukumu ya kulinda mipaka, katiba na kumtii mkuu wa nchi,  wanatumia fursa ya udhaifu wa uongozi serikalini kwa kushindwa kutimiza matakwa ya wapiga kura, hali ambayo husababisha kelele na manung’uniko kutoka kwa wananchi, ndipo wapiga kwata hutumia nafasi hiyo kupindua huku wakijitetea kuwa wamefanya hivyo ili kuwasaidia wananchi wanaokandamizwa. 

Pia inasadikika hata makundi ya kigaidi yanayoibuka mara kwa mara katika baadhi ya mataifa yanatokana na mgawanyo usio sawa wa rasilimali za nchi.

Hata hivyo, mapinduzi ya kijeshi hayakubaliki hata kidogo katika dunia hii iliyostaarabika na yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote. 

Wanajeshi wanatakiwa kubaki kambini wakitimiza majukumu yao ya msingi ya kulinda mipaka ya nchi, katiba na utii kwa viongozi wa serikali walioko madarakani na si vinginevyo. 

Zipo njia chanya za kuwasulubisha viongozi wa serikali wababaishaji wasiowajibika lakini si kwa mapinduzi haramu ya kijeshi.

0756521119

By Jamhuri