Giza nene Ngorongoro

Na Mwandishi Wetu

Wakati serikali na wadau wa uhifadhi ndani na nje ya nchi wakihaha kuikokoa Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) isitoweke, imebainika kuwa baadhi ya vigogo, wakiwamo wabunge, wanamiliki maelfu ya mifugo katika eneo hilo.

Tayari kampeni kubwa imeanza kwa kuwatumia baadhi yao kukwamisha mpango wa serikali wa kudhibiti idadi ya watu na mifugo ili kuinusuru Ngorongoro.

Kwa miaka mingi JAMHURI limesimama kidete kuhadharisha juu ya hatari inayoikabili NCAA na Pori Tengefu la Loliondo kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.

 Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa wakati wa sensa maalumu iliyofanywa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali katika eneo la Ngorongoro mwaka 2017; mbunge mmoja na mwenzake ambaye hakurejea bungeni, kila mmoja alikuwa na wastani wa ng’ombe 2,000 ndani ya NCAA na katika Pori Tengefu la Loliondo.

Ripoti hiyo ya sensa imesheheni mambo mengi yanayothibitisha kuwa ng’ombe, mbuzi na kondoo waliojaa Ngorongoro ni mali ya viongozi na matajiri wachache.

Mathalani, ilibainika kuwa asilimia 80 ya mifugo yote inamilikiwa na asilimia tatu pekee ya watu -wengi wao wakiwa wanaishi nje ya eneo hilo. Watu wengi wanaochunga mifugo hiyo ni waajiriwa ambao ujira wao mara nyingi ni maziwa.

Aidha, imebainika kuwa ng’ombe wengi wanaingizwa nchini wakitoka Kenya ambako baadhi ya viongozi wa vijiji wilayani Ngorongoro huingia makubaliano. Wakiingia nchini hunenepeshwa na kisha kuuzwa katika mnada wa Posmolu, ambako wanunuzi wakuu ni raia wa Kenya.

“Ripoti ilieleza kila kitu, Baraza la Wafugaji lilishirikishwa mwanzo hadi mwisho, lakini halitaki ripoti hiyo kwa sababu imesheheni ukweli mwingi sana,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:

“Ninaposikia kwamba kunafanyika vikao au utafiti, najiuliza utafiti na taarifa gani zaidi? Nakuhakikishia kuwa tatizo ni uamuzi, si taarifa za ukweli wa mambo ulivyo.”

Mwaka 2007 kaya 159 zilihamishwa kwa hiari kutoka NCAA na kupelekwa Kata ya Oldonyosambu, Tarafa ya Sale.

“Wakaanzisha Kijiji cha Jema… hiki ni miongoni mwa vijiji bora kabisa Tanzania… wakawekewa miundombinu na huduma zote za kijamii. Mashamba ekari 3 kila familia, hospitali ya kisasa, shule ya kisasa ya msingi, barabara, mradi wa maji na kila kitu.

“Hadi mwaka 2021 watu wa kaya zaidi ya 80 walikuwa wamerudi tena ndani ya hifadhi! Na waliowashawishi kurudi ni hao hao ambao walikuwa kwenye kamati ya kuwahamisha wakiongozwa na kiongozi mkuu wa wilaya wa CCM, viongozi wa Baraza la Wafugaji na diwani wa kata mojawapo,” kimesema chanzo chetu.

Baraza la Wafugaji ambalo lilikuwa likipewa mgawo wa moja kwa moja wa wastani wa Sh bilioni 4 kwa mwaka, fedha hizo ziliishia mifukoni mwa wachache, hasa viongozi.

“Fedha hizo zinatafunwa tu na ndiyo maana mwaka 2018 Mama Samia Suluhu Hassan alipokwenda NCAA aliwauliza (Baraza) kuwa wanafanya nini na hizo pesa ikiwa zinazidi mara mbili bajeti ya maendeleo ya Halmashauri ya Ngorongoro? Hawakutoa majibu.

“Kelele unazozisikia eti za kutetea watu wasiondolewe ni mbinu tu za wakubwa kutaka waendelee kufaidi fedha, lakini pia ni eneo la malisho. Serikali iamue sasa kwamba Ngorongoro inabaki kuwa eneo la uhifadhi ili kunusuru rasilimali ya wanyamapori na malikale,” amesema mmoja wa watumishi waliowahi kufanya kazi Ngorongoro.

Wakati Ngorongoro ikizaliwa mwaka 1959 kulikuwa na watu 8,000 na hadi mwaka 1974 ilipoundwa NCAA idadi hiyo ilikuwa imepanda hadi watu 24,000. Mwaka huu wa 2022 inakisiwa kuwa idadi ya watu ni zaidi ya 100,000.

“Sasa leo una watu zaidi ya laki moja, tena wanaohitaji umeme, nyumba za block, baa, masoko, kuendesha kilimo, kuchoma mkaa na kuendesha bodaboda eti ndani ya hifadhi na kila aina ya maisha ya kisasa…je, balance (uwiano) inaendelea kuwapo? Hoja si kwamba kusiwe na wakazi na mifugo ndani, hapana; hoja ni kuwe na watu wangapi, na mifugo mingapi?

“Serikali ina lawama kwa upande mmoja kwa sababu mambo mengine ndiyo inachochea. Kwa mfano, unajua vijiji vyote 25 vilivyo ndani ya NCA vipo kwenye mradi wa REA III? Unapeleka umeme ambao ni chanzo cha maendeleo mengine ya kisasa halafu unataka hifadhi ibaki salama! Eti hiyo ndiyo hifadhi, ajabu sana,” kimesema chanzo chetu.

Kwa sensa ya mwaka 2017, Tarafa ya Ngorongoro ilikuwa na ng’ombe 238,826. Kata za tarafa hiyo na idadi ya ng’ombe kwenye mabano ilikuwa kama ifuatavyo: Endulen (32,273; asilimia 13.5) Ngorongoro (31,387; asilimia 13.1), Nainokanoka (28,718; asilimia 12), Kakesio (26,998; asilimia 11.3), Alailelai (20,728; asilimia 8.7), Naiyobi (18,672; asilimia 7.8) na Alaitolei (18,275; asilimia 7.7). Kata zilizokuwa na idadi ndogo ya mifugo zilikuwa Olbalbal (14,790; asilimia 6.2), Ngoile (14,993; asilimia 6.7), Eyasi (15,145; asilimia 6.3) na Misigiyo (16,847; asilimia 7.6).

Maneno ya Mwalimu Nyerere

Septemba, 1961 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitamka maneno maarufu ambayo kwa miaka mingi kabla ya sheria mpya za uhifadhi ndiyo yaliyokuwa na yanaendelea kuwa dira ya kulinda rasilimali wanyamapori na misitu.

Maneno hayo hadi leo yanatumiwa na wenye dhamama ya kulinda maliasili ya wanyamapori kama mwongozo na hamasa kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na viumbe wengine. Mwalimu Nyerere alisema: “Kudumisha uhai wa wanyamapori wetu ni suala linalotuhusu sana sisi sote katika Afrika. Viumbe hawa wa porini pamoja na mapori wanamoishi si tu kwamba ni muhimu kama mambo ya kustaajabisha na kuvutia, bali pia kwamba ni sehemu muhimu ya maliasili yetu na ustawi wa maisha yetu katika siku za baadaye.

Kwa kukubali dhamana ya kuhifadhi wanyama wetu tunatoa tamko la dhati kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu na watoto wetu wataweza kufaidi utajiri na thamani ya urithi huu.

Kuhifadhi wanyamapori na mapori waishimo kunahitaji utaalamu maalumu, watumishi waliofunzwa pamoja na fedha. Tunatazamia kupata ushirikiano kutoka kwa mataifa mengine katika kutekeleza jukumu hili muhimu. Kufanikiwa au kushindwa kwa jukumu hilo kutaathiri si tu Bara la Afrika pekee, bali ulimwengu mzima.”

Maneno hayo yamekuwa chachu na hamasa kwenye uhifadhi wa wanyamapori. NCAA imeendelea kuutumia mwongozo huu wa Mwalimu Nyerere, na viongozi wakuu wengine wa nchi yetu kama dira ya utendaji kazi wake.

Sheria iliyoanzisha NCAA mwaka 1959 imekipa chombo hicho dhima kuu tatu: Mosi, kusimamia uhifadhi wa wanyamapori na malikale; Pili, kuendeleza wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi, na Tatu, kuendeleza utalii.

“Mamlaka ya Ngorongoro imeendelea kusimamia dhima hizi ili kuhakikisha kuwa urithi huu unaendelea kudumu kwa faida ya Watanzania na walimwengu wote,” amepata kusema Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dk. Freddy Manongi.

Mwalimu Nyerere hakuchoka kuonya juu ya athari zinazosababishwa na uuaji wa wanyamapori na uharibifu wa mazingira.

Akizungumza na viongozi wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na watumishi wa serikali mkoani Kilimanjaro; Agosti 10, 1975 Mwalimu alieleza mambo yanayowagharimu watu wa mataifa ya Ulaya na Marekani baada ya kuua wanyamapori na kuharibu misitu. Ikumbukwe kuwa miaka mia kadhaa iliyopita Ulaya na Marekani walikuwa na wanyamapori wengi, uharibifu wa kibinadamu umewateketeza.

Mwalimu akiwahutubia wanachama hao wa TANU alisema: “Ni vizuri kujifunza kwa wenzetu waliotangulia. Na wakati mwingine ni kujifunza kutokana na makosa yao. Wenzetu waliotangulia tunaowasema zaidi ni wale wa nchi zilizoendelea sana hasa za Ulaya na Amerika Kaskazini.

“Wamefanya makosa mawili makubwa – wao wanajua, sisi hatujui. Wao wanajua kwa sababu wameyafanya makosa hayo, sisi kwa sababu hatuyafanya hatujui kwamba ni makosa. Moja mtashangaa nikilitamka. Wameharibu sana nchi zao kwa kitu wanachokiita maendeleo. Wameua vi-nyama vingi sana vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu – vingi. Wameua vyote. Hawana tena makundi makubwa makubwa ya wanyama kama tuliyonayo katika Afrika na hasa katika Tanzania. Hawana kabisa.

“Sasa wao wanajua kwamba wamefanya makosa, na wanakuja huku wanatwambia: ‘Sisi tumefanya makosa, tumeua wanyama wetu wote tumemaliza, tafadhalini msiue wanyama wenu.’ Sisi tunawaona kama wajinga wanapotuambia hivyo. Lakini wao wanajua kosa kubwa la kufuta wanyama na kuwamaliza; na kukatakata misitu yao na kuimaliza. Wanajua kosa walilolifanya na wanatuomba tusilifanye kosa hilo.

“Sasa wanakuja kwa wingi, ndio hao mnawaita watalii. Wanakuja kwa wingi kuja kuona wanyama. Wewe unamshangaa huyu mtu mzima anatoka kwao mbaaaaali kuja… anatoka kwao mbaaaali, analipa hela kuja kuona tembo, kwanini? Ana akili, hana akili? Ni kwa sababu ana akili ndiyo maana anatoka kwao mbali sana, analipa fedha anakuja kuona tembo. Angekuwa hana akili asingekuja. Anajua faida ya kuwa na ma-tembo, na ma-simba, na ma-nyati, na ma-chui, na ma-pundamilia katika nchi hii, lakini kwao wameshafuta. Sasa wanaanza kutuomba, wengine wanaanza kutuomba tuwauzieuzie angalau wafufuefufue, lakini kufufua si jambo jepesi. Ukishaifuta misitu, kuifufua na kuweka wanyama waishi kama walivyokuwa zamani ni vigumu sana. Kwanza hali yake ile ni tofauti. Huwezi kuifufua, vigumu sana. Wala hawajui ilikuwaje hata waweze kuifufua. Sasa nasema wanatushawishi – Wazungu wanatushawishi katika jambo hilo ambalo hatujafanya kosa, tusifanye kosa.

“Serikali ya Tanzania imekubali, nadhani wananchi wanaanza kukubali kutofanya kosa hilo lililofanywa na wenzetu. Tuhifadhi wanyama wetu na tuhifadhi misitu yetu. Tusivuruge vuruge mazingira ambayo tumeyarithi, na kwa kweli hatujui yamechukua muda gani hata yakawa hivyo; halafu tunafika sisi tunaita maendeleo tunavuruga vuruga, tunaharibu; tunaua wanyama, tunakata miti. Matokeo yake hatuwezi kuyajua.” Mwisho wa kunukuu.

Mapema mwaka jana, Rais Samia akihutubia wakati wa kuwaapisha mawaziri, aliagiza kushughulikiwa kwa matatizo yanayotishia kutoweka kwa Ngorongoro. Aliwaagiza viongozi wahusika kuamua moja kati ya haya, ama kuacha Ngorongoro ife, au kuchukua hatua za kuiokoa.

Tangu atoe agizo hilo, juhudi za kuikoa Ngorongoro zimekuwa zikichukuliwa ikiwa ni pamoja na mikutano na semina kwa wadau mbalimbali.

Hata hivyo, mpango huo unakosolewa na baadhi ya watu wanaoamini kuwa ripoti za kitaalumu zilizopo, pamoja na ushirikishwaji wananchi uliokwisha kufanywa na mamlaka mbalimbali, vilitosha kuwa dira ya kuziokoa Ngorongoro na Loliondo.